MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Viongozi wa Taasisi na Mashirika wanawajibika kuchangia juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuandaa na kutekeleza mikakati itakayosaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni unaofanyika katika Ukumbi wa APC – Mbweni Jijini Dar es Salaam.
Alisema, Mikakati itakayoandaliwa ni vema ijielekeze katika kuhimiza matumizi bora ya rasilimali, uwekezaji katika nishati mbadala na teknolojia rahisi na nafuu, na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Kuhusu Biashara ya Kaboni, Makamu wa Rais alisema ni muhimu kuwepo kwa uratibu madhubuti katika utekelezaji wa biashara ya kaboni kwa kuwa biashara hiyo inahusisha wadau wengi.
Aliongeza, ni vema Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Serikali za Mikoa kukutana kwa ajili ya kujadili na kupata mwelekeo wa pamoja katika uendeshaji wa biashara hiyo.
Pia, Makamu wa Rais alisema ni muhimu kupata uzoefu kuhusu uendeshaji wa biashara ya kaboni kutoka nchi nyingine ili kuona namna zinavyokabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Makamu wa Rais alisema uwazi katika mikataba ya biashara ya kaboni utasaidia uendeshaji wa biashara hiyo na kuondoa hali ya kutoaminiana.
Dkt. Mpango alisema kwa sehemu kubwa, uendeshaji wa biashara hiyo umetawaliwa na Madalali ambao pia utaratibu wa upatikanaji wao hauko wazi.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufahamu kilicho ndani ya mikataba kati yao na wanunuzi na kama kiasi kinacholipwa ndicho kilichotolewa na wanunuzi.
Makamu wa Rais alisema, taratibu za jinsi biashara ya kaboni inavyofanyika zinapaswa kuwekwa wazi kwa wadau wakuu, yaani Wanavijiji na Halmashauri, ambao ndiyo wamiliki wa misitu.
Alisisitiza, Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na TAMISEMI kuongeza kasi ya kufanya programu maalum ya kufikisha elimu katika ngazi ya wilaya na vijiji. Pia ameviagiza Vyombo vya Habari na Taasisi za Teknolojia kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya biashara ya kaboni.
Halikadhalika, Makamu wa Rais alisisitiza taasisi na mashirika kutekeleza mipango ya kutumia vifaa vyenye matumizi kidogo ya umeme na kuhamia kwenye magari yanayotumia umeme na gesi.
Amewasishi Wakuu wa Mikoa kuhamasisha vyombo vya ulinzi na usalama katika mikoa kuanza kutumia magari yanayotumia nishati ya umeme na gesi.
Alisema, ni muhimu taasisi na mashirika yawe na vitengo vya mazingira na kutenga bajeti za utekelezaji wa miradi na shughuli za kuhifadhi mazingira.