Mikutano, midahalo yaimarisha uhusiano wa Jeshi la Polisi na waandishi wa habari

0

Na Iddy Mkwama

UHUSIANO na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari nchini kwasasa umeimarika zaidi kufuatia mikutano na midahalo ambayo imefanyika kwenye ngazi mbalimbali nchini.

Msemaji wa Jeshi la Polisi ACP David Misime alisema hayo wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya habari kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, uliofanyika Novemba 18, Mlimani City Jijini Dar es Salaam na kuwahusisha Wahariri na Makamanda wa Polisi wa Mikoa mbalimbali nchini.

Misime alisema, wamefanikiwa kushiriki midahalo mitano ambayo imehusisha waandishi wa habari, pia mikutano 50 kwa ngazi ya mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, ambapo ilihudhuriwa na washiriki takribani 1,500 kwenye mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani.

Alisema, lengo la kufanyika kwa mikutano hiyo ni kuhakikisha changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza baina ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi zinamalizika kwa ajili ya maslahi ya nchi.

Misime alisema, kila mmoja anamuhitaji mwenzake katika kutekeleza majukumu yake, “mimi nauhitaji sana mwandishi wa habari, navihitaji sana vyombo vya habari ili yale tunayoyafanya wananchi wajue majukumu ya Jeshi la Polisi, kama kuna tukio limetokea wapate taarifa sahihi ya nini kilichofanyika, wapate tahadhari kama kuna matishio ya kiusalama,”

Alisema, mwandishi wa habari anawahitaji walinzi wa usalama ili afanye kazi yake akiwa salama, “tunafanya mikutano hii ili kuhakikisha manung’uniko yanaondoka, tuwe na ukurasa mpya, tusonge mbele kama Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano anavyotutaka tufanye kazi kwa mashirikiano,”

Misime alisema, kupitia mikutano na midahalo ambayo wameshiriki kwa ngazi ya Kitaifa, wamezungumza mengi na alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC) na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kwa kufanikisha jambo hilo.

“Tumeboresha mahusiano yetu na waandishi wa habari, kusema ukweli mahusiano ni mazuri sana, ukiona mtu anazungumza tofauti sasahivi, ni mtu ambaye anazungumzia historia, tulishatoka huko, tupo mbali,” alisisitiza Misime.

Aidha, Misime alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha waandishi wa habari juu ya wajibu wao wakati wa uchaguzi ambapo alisema, ni vema wakazingatia maadili ya taaluma yao, wakawa mstari wa mbele kutunza na kuhamasisha amani na kujiepusha kutoa taarifa za uchochezi.

“Wajibu mwingine wahakikishe taarifa zinazohusu uchaguzi, zinabeba ukweli ili kuepuka taarifa chonganishi zinazoweza kuleta vurugu kama ilivyowahi kutokea kwenye nchi nyingine.”

“Vile vile watoe elimu inayohusiana na sheria, kanuni na wajibu wa mpiga kura, kuhamasisha uzalendo, amani, utulivu na usalama sababu hiyo ndio misingi yetu inayotufanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani,” alisema.

Mbali na hayo, alisema waandishi wanapaswa kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara juu ya usalama na kupatiwa vifaa kama vile makoti yenye nembo ya utambulisho.

“Mara nyingi inapotokea sintofahamu kati ya polisi na waandishi, unakuta baadhi hawana hata makoti, hawana vitambulisho, anakuambia si unaona nina kamera? Sasahivi kila mtu ana kamera, kwahiyo tunasisitiza vyombo vya habari kuzingatia hilo na kuwapa waandishi mafunzo ya usalama,” alisema.

Pia, Misime akisisitizia suala la mafunzo kwa waandishi wa habari alisema, kwenye mikutano ambayo wameshiriki waliahidi kutoa mafunzo ili wadau hao wajue namna ya kujilinda wanapokwenda kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo ambayo sio salama.

“Kwamba wajue wanapokwenda mahala kwenda kuripoti na kuna viashiria vya vurugu, wasimame upande gani, kusimama upande ambao unataka uone bomu la machozi linavyotoka ili upate picha nzuri sio sawa, unaweza kupata madhara na linaweza kukumaliza wewe,”

“Ukiambiwa unasema ‘Wananchi wana haki ya kupata taarifa sahihi’, mfuate Kamanda amesimama upande gani, fuata taarifa kwa kulinda usalama wako, vita havina macho, kwahiyo hilo tunalifanya ili muwe salama,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi alizitaka pande zote mbili; Jeshi la Polisi na waandishi wa habari nchini, kila mmoja kuheshimu mipaka ya mwenzake wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kulinda usalama wao na wananchi kwa ujumla.

“Tukiheshimiana, tukitekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria, wote tutakuwa salama, aidha niwakumbushe usalama wako na wangu, unaanza na wewe, umetumwa na chombo cha habari, hata kama umebeba kamera, zingatia hapo unapokwenda pakoje? Ukienda ukikutana na Kamanda muulize, kwamba hapa tunapokwenda kuna sintofahamu, nifanyeje? Usalama kwanza, mengine yanafuata,” alisema Misime.

Awali, akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya, alisema mikutano ambayo wameifanya na Jeshi la Polisi kwenye baadhi ya mikoa, ina mwelekeo mzuri na wamepiga hatua kubwa tofauti na ilivyokuwa kabla ya mikutano hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wahariri na waandishi wa habari waliozungumza kwenye mkutano huo na baada ya mkutano, walishukuru hatua ya Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya habari kwa kuwakutanisha na makamanda hao, huku wakilipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanya mikutano kwa ajili ya kujadili changamoto zinazosababisha kuimarisha mahusiano yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here