WAZIRI wa Kazi,Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amefanya ziara ya siku mbili mkoani Mwanza ikiwa na lengo la kukagua maandalizi ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru ambao utahitimisha mbio zake Oktoba 14, katika uwanja wa CCM Kirumba.
Akiwa jijini Mwanza, Waziri Kikwete amepata nafasi ya kukutana na makundi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa kilele hicho na wiki ya Vijana ambayo inatarajia kuanza Oktoba 8 hadi 13, 2024 katika viwanja vya furahisha.
Waziri Kikwete ambaye alikutana na makundi ya Vijana Wasanii katika fani mbalimbali na baadae kukutana na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Walimu wa sekondari na vyuo toka wilaya zote za Mkoani humo,alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru pamoja na kushiriki kilele cha wiki ya vijana.
Baada ya mikutano hiyo ya Wadau, Waziri Kikwete alifika Uwanja wa CCM Kirumba kuona maandalizi ya halaiki, ambapo alishuhudia vijana wakiendelea na maandalizi yao na katika salamu zake aliwapongeza walimu wa vijana hao na kuwatia moyo wanafunzi ambao wameandaliwa vizuri.