IMEELEZWA kuwa, hatua ya kuongeza bidhaa za utalii ikiwemo mbio za Marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa, zimekuwa zikivutia washiriki wengi na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo husika.
Kamishna Mkuu wa Uhifadhi Mussa Kuji alisema hayo jijini Dar es Salaam, na kutaja hifadhi zilizofanikiwa kuratibu mbio za Marathoni ambapo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi – Chato na Kilimanjaro.
“Kumekuwepo na ongezeko la bidhaa za utalii katika maeneo mengine ambayo awali hayakuwa na bidhaa husika, Kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto (balloon) kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa hifadhi ya Mikumi,” alisema Kuji.
Aidha, Kuji alisema bidhaa nyingine ambazo zimeongezwa na kuvutia watalii wengi, ni Utalii wa faru (Hifadhi ya Taifa Mkomazi), utalii wa baiskeli (Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha); Utalii wa michezo na burudani (Hifadhi ya Taifa Serengeti – Mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi – Mpira wa miguu, pete na kikapu).