ICTC inavyochagiza kasi ya Tanzania ya Kidijitali

0
Mkurugenzi wa Tume ya Tehama, Nkundwe Mwasaga.

Na Iddy Mkwama

SERIKALI ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeonekana dhahiri imejipanga kuendana na kasi ya dunia ambayo kwa sasa shughuli nyingi zinafanyika kwa njia ya Kidijitali.

Ndio maana, katika kufikia lengo hilo, Serikali imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuboresha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini ili kuhakikisha huduma za malipo kwenye sekta ya afya sambamba na matibabu, uzalishaji, kilimo, uchimbaji wa madini na nyinginezo, zinafanywa kwa njia za Kisasa.

Ni wazi kwamba, TEHAMA imesaidia masuala mbalimbali hapa nchini ikiwemo huduma za fedha kupitia benki; ambapo mwananchi anaweza kufanya shughuli za kibenki bila kufika benki na hilo limesaidia kupunguza foleni kwenye mabenki na kuokoa muda mwingi ambao ulikuwa unapotea.

“Kabla ya kuanzishwa kwa huduma hizi za kisasa kwa mfumo wa Kidijitali, ilikulazimu kutenga siku nzima kwa ajili ya kwenda kupata huduma benki, kwa kweli tulikuwa tunapoteza muda mwingi sana, leo unakaa tu ofisini, nyumbani au popote ulipo, unapata huduma ambazo ilikulazimu kwenda benki ili uzipate,” anasema Juma Mponda, mkazi wa Pugu, Dar es Salaam.

Mponda alipongeza jitihada za Serikali katika kuhakikisha lengo la kuifanya Tanzania kuwa ya Kidijitali linafanikiwa, ambapo mpango huo upo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, huku Msimamizi Mkuu ni Tume ya TEHAMA (ICTC).

Tume ya TEHAMA ilianzishwa Novemba, 2015 ambapo ilianzishwa kufuatia Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 iliyoidhinishwa na Serikali Machi, 2003 ambayo ilielekeza kuanzishwa kwa chombo katika Mfumo wa Kitaasisi wa sekta hiyo ili kuratibu na kuwezesha sera na utekelezaji wake nchini.

Majukumu Makuu ya Tume ya TEHAMA ni kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA katika sekta binafsi na Taasisi za Serikali, pia kukuza TEHAMA kwa kuwawezesha wataalamu wenye uwezo katika kufanya shughuli zote zinazohusu TEHAMA nchini.

Mbali na majukumu hayo, ICTC inapambana kuifanya Tanzania kushindana Kidunia katika utekelezaji shughuli za TEHAMA. “Hadi sasa tume imeshasajili wataalamu wa TEHAMA 1,600 wanaohudumia nchi nzima,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga.

“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika TEHAMA, kwani hapa nchini kampuni mbalimbali zimetengeneza mitaji mikubwa na zinafanya kazi nchi nyingi duniani,”

Katika kuthibitisha kwamba ICTC, imepania kutimiza malengo ya Serikali kwenye upande wa TEHAMA na inaweka mizizi kwenye sekta hiyo, Dkt. Masaga anasema, Serikali inakusudia kujenga vituo nane (one-stop centres) nchini vya ubunifu wa teknolojia vitakayowezesha vijana na wananchi kwa ujumla kuvitumia kuboresha kazi zao za kibunifu.

Vituo hivyo vinatarajiwa kujengwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Tanga, Mwanza, Mbeya na Zanzibar. “Huu ni mpango wa awali, lakini mkakati uliopo ni kujenga vituo katika mikoa yote na wilaya zote ili wananchi waweze kuvitumia na kujifunza suala zima la teknolojia.”

Aidha, anasema vituo hivyo vitajengwa katika maeneo karibu na vyuo na shule ambavyo vitasaidia vijana nchini kubuni na kuanzisha kampuni changa za ubunifu wa vitu mbalimbali vinavyohusiana na teknolojia na kuviendeleza, ambapo vitakuwa na uwezo wa kuingiza watu 200 kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, aliwaomba wadau mbalimbali kushirikiana katika kuanzisha vituo hivyo ambavyo ni sehemu ya vipaumbele 13 vya ICTC vilivyowekwa ili kuleta mapinduzi ya teknolojia na ubunifu nchini; lengo likiwa ni kukuza vipaji tofauti.

“Tunatarajia kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT Refurbishment and Assembly Centre) na vituo vya majaribio vya ubunifu TEHAMA (District ICT Startups Innovation Hubs) katika wilaya 10.”

Vile vile, tume hiyo tayari imeanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT refurbishment and assembly centre) sambamba na kuwezesha mafunzo maalum ya TEHAMA kwa wataalamu kukuza na kuendeleza ujuzi wa TEHAMA nchini.

Kwa upande mwingine Dkt. Mwasaga aliweka wazi kwamba, wanatarajia kujenga kituo kwa ajili ya akili bandia au akili mnemba (Artificial Intelligence – AI).

Teknolojia hiyo ambayo imekuwa gumzo duniani kote, hapa nchini imezua hofu kubwa ambapo watu wengi wanaamini inaweza kuwakosesha kazi iwapo itaanza kutumika, jambo ambalo Dkt. Mwasaga anasema halina ukweli, kwani akili bandia inaleta tija na kwamba watu wakipewa ujuzi mpya kuhusu teknolojia hiyo, itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi.

“Tutajenga kituo cha Artificial Intelligence kwa ajili ya kuendeleza wataalamu wa TEHAMA pamoja na kuwezesha mafunzo maalum ya wataalamu wa TEHAMA 500 ili kukuza na kuendeleza ujuzi wa TEHAMA nchini,” anasema Dkt. Mwasaga.

Mbali na ujenzi wa vituo hivyo, ICTC katika jitihada za kuendelea kujenga msingi imara, imewezesha mijadala miwili (2) ya wadau kutoka sekta ya Umma na Binafsi inayohusu maboresho ya sheria katika sekta ya TEHAMA na kuvutia uwekezaji ili kuharakisha ukuaji wa sekta kwa kuihusisha sekta binafsi.

“Mijadala ya TEHAMA na Sekta binafsi imeiwezesha Tume kusaini mikataba ya maelewano ya uwezeshaji katika TEHAMA na Mashirika na taasisi mbalimbali zikiwemo Benki ya CRDB, UNCDF, UNDP, DOT na UNESCO,” anasema Dkt. Mwasaga.

Mkurugenzi huyo anasema, wanajivunia na hatua waliyofikia ya kutengeneza mfumo Jumuishi utakaounganisha usajili na uendelezaji wa wataalamu na wabunifu TEHAMA nchini (ICT human capital development system).

Lengo la mfumo huo ni kutambua bunifu na kupanua wigo wa ukuzaji wa wabunifu na bidhaa na huduma za TEHAMA zinazozalishwa Tanzania na hivyo kukuza pato la Taifa na kuongeza fursa za ajira kupitia TEHAMA na maendeleo ya Kidijitali duniani.

“Pia tuliandaa mkutano wa mwaka wa TEHAMA (TAIC) na Tuzo ya TEHAMA Tanzania (Tanzania ICT Award), hili lilikuwa kongamano kubwa la mwaka la TEHAMA lililofanyika Zanzibar mwezi Oktoba, 2022 na kuwashirikisha wawekezaji na wadau mbalimbali wa TEHAMA kutoka ndani na nje ya nchi wapatao 1,200,” anasema.

Anasema, watafanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA nchini na kufanya tathmini ya Kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya TEHAMA.

Aliongeza kwamba, wataratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za TEHAMA ndani na nje ya nchi. “Tutashirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za TEHAMA ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za TEHAMA hapa nchini.”

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwasaga anasema, wamejipanga kuhakikisha wanakuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogo ndogo (startup) kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za ‘startups’ duniani.

Anasema, Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na wabia mbalimbali nchini ili kuwawezesha vijana wenye kampuni kupata fursa zitakazosaidia ukuaji wao kiuchumi na jitihada za wabia hao zimeanza kuonekana na kuzaa matunda.

Moja ya jitihada hizo ni uwepo wa mradi wa Funguo ambao hivi karibuni ulitangaza dirisha la pili la Mradi wa Funguo ambao walikabidhiwa Shilingi Bilioni 1.2 kupitia Mradi uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa.

Meneja mradi wa Funguo Joseph Evarist Manelukiza akizungumza mara baada ya kuwatangaza washindi hao alisema, kupitia kampuni changa zinazomilikiwa na watanzania, watahakikisha wanaboresha Mazingira ya Biashara, Ukuaji na Ubunifu na kuwawezesha wabunifu ambao wanaanza ili waweze kuendesha biashara zao na ziweze kusonga mbele.

“Jukumu kubwa la Mradi wa Funguo ni kuwezesha makampuni machanga ya Wabunifu wanaoibukia kwa kutoa mitaji wezeshi ili waweze kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine,” anasema Manelukiza, huku akiwataka wale waliokosa fursa hiyo kwa awamu hii, wasikate tamaa, kwani wataunganishwa na taasisi nyingine ili wapate mitaji.

Anasema, Awamu ya kwanza walioomba na kupata mtaji ni 26 na Awamu ya pili wamepata 17 ambapo wamepata jumla ya Shilingi Bilioni 3.8.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema “Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo katika sekta zote lakini kwa kutumia teknolojia ambazo zitachagiza maendeleo hapa nchini.

Ni dhahiri mafanikio ambayo Tume ya TEHAMA wameyapata kwa takribani miaka miwili iliyopita na malengo yaliyowekwa, kwa miaka michache ijayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kwenye sekta ya TEHAMA na kukimbizana na kasi ya ulimwengu wa Kidijitali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here