Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Simba imedhamiria kuionyesha Afrika uzinduzi wa jezi mpya itakayotumiwa katika msimu wa mwaka 2023/2024 tukio hilo ambalo litafanyika katika katika Kilele cha Afrika Mlima Kilimanjaro maarufu Paa la Afrika.
Zoezi ambalo linategemewa kufanyika Julai, 21 katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Mita 5895 kutoka usawa wa bahari.
Akizungumza katika hafla kuwaaga wa wapandaji Mlima kupeleka jezi hizo katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Abdallah Mwaipaya aliwapongeza Klabu ya Simba kwa ubunifu huu na uzalendo wa kuitangaza nchi.
Ni tukio kubwa ambalo Klabu ya Simba wameweza kuongeza thamani ya Mlima Kilimanjaro na utalii kwa ujumla wa nchi yetu niwatake mashabiki wote wa Simba waliopo katika mikoa ya karibu na Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi kuwapokea wapandaji Mlima wanaporejea siku ya jumamosi” alisema Mwaipaya
Naye, Msemaji wa Simba SC Ahmed Ally alisema “Jezi zetu zitazinduliwa Julai, 21 2023 Juu ya Mlima Kilimanjaro kwenye Kilele cha Uhuru saa 1:00 Usiku tukio litakua Live kutoka Mlimani,”
Pia, Ahmed Ally alielezea sababu za jezi ya Simba SC kuzinduliwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro ni kuwa klabu ya Simba imekuwa na maono ya kuiunga mkono serikali kwenye kutangaza na kukuza utalii wa ndani.
“Nyote mnafahamu kwa muda wa miaka mitano sasa tumekuwa tukitumia utambulisho wa ‘VISIT TANZANIA’ katika jezi zetu na katika jezi ya msimu uliopita ilikuwa na alama ya Mlima Kilimanjaro hii ni ishara kwamba Simba tupo bega kwa bega na Serikali kupigania utalii wa nchi yetu,” alisema.
Vile vile, Ahmed Ally aliongeza kuweka nembo za mlima katika jezi Klub ya Simba iliona haitoshi na kuamua ni lazima Afrika na Dunia nzima kuona jezi hiyo na kutambulisha utalii na Mlima wetu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro Afisa Uhifadhi Mkuu, Mapinduzi Mdesa alitoa rai kwa klabu zingine nchini kuiga mfano wa Klabu ya Simba nakuja na mawazo mengine ya kutangaza utalii wetu.
“Huu ni ubunifu ambao Klabu ya Simba imekuja nao kama Hifadhi tunachukulia ni jambo zuri sana katika kutangaza utalii wa ndani hivyo kupitia zoezi hili tunaimani kwamba inaenda kuhamasisha watanzania wengi lakini pia waafrika na watu wote duniani kuvutiwa kupanda Mlima Kilimanjaro, nitoe wito kwa klabu zingine kuja na ubunifu wao kupitia maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kuja kufanya hamasa kwa mashabiki wao na kwa watanzania kwa ujumla,” alisema.