Na Dkt Ahmad Sovu
TRENI ya Kigoma wengine huita gari moshi au chuma cha Mjerumani au gogo vyovyote iitwavyo, imekuwa chombo cha usafiri mkombozi katika mikoa ipitayo Bara hasa Tabora na Kigoma.
Katika kuwajali na kuwathamini wananchi wake wanaotumia usafiri huo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya Awamu ya Sita, ilinunua mabehewa mapya ya Kisasa 22 ya Meter Gauge Railway (MGR) na vichwa 3 kupitia mradi wa uboreshaji wa reli ya kati.
Tumeshuhudia Disemba 15, 2022, mabehewa hayo yakianza kutumika kwa kuanza safari zake kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora na Kigoma.
Hali hiyo ilionesha furaha kubwa kwa abiria walikuwamo kwenye treni hiyo. Mmoja alisikika akisema ‘Asante Mama Samia hali hii ikiendelea hatutapanda tena mabasi.’
Hisia kali za mwananchi huyu kwa Rais Samia imenitia hamu kuelezea japo kwa muhtasari faida zitakazopatikana kwa mwananchi Mnyonge ambaye usafiri wa treni kwake ndio tegemeo.
Mosi, kupata uhakika wa safari zao kwa mwananchi wa kawaida kuanza kutumika kwa mabehewa haya mapya na vichwa vipya vya treni tayari, vinamtoa hofu na kumhakikishia kuwa, usafiri wa treni sasa ni imara.
Hivi sasa zitakwenda bila shaka wala mashaka yoyote yale. Maana moja ya sababu iliyokuwa ikielezwa hapo awali wakati kukiwa na changamoto za kukosekana kwa usafiri wa uhakika, ni upungufu wa mabehewa ya kutosha. Sasa Dkt. Samia kayaleta, uhakika wa safari pia upo!
Pili, usafiri wa kisasa kwa bei ileile, hii inaufanya usafiri huu kuendele kuwa nafuu kuliko aina nyingine za usafiri kama vile mabasi na ndege. Pia, mbali na unafuu wa bei, mabehewa yake i ya kisasa na yana kila aina za huduma muhimu kwa wasafiri.
Mfano kwa sasa, nauli daraja la tatu ni Shilingi 35,700 tu, ambapo kwa usafiri wa mabasi ni kati ya Shilingi 50,000 hadi 70,000. Kwa mantiki hiyo, Dkt. Samia anashuka kabisa kwa wananchi wa hali ya chini na kuhakikisha wanapata huduma bora na za kisasa kwa bei nafuu kabisa.
Tatu, kutoa fursa ya ajira kwa wananchi wanyonge akina mama na vijana wajasiriamali. Wale wanaosafiri kwa treni mara kwa mara au japo mara machache watakubaliana na mimi kuwa, kuongezeka kwa idadi ya safari za treni kutaongeza ajira na fursa ya biashara kwa wananchi wa kawaida kabisa.
Kwa kawaida, pembezoni mwa vituo mbalimbali vya treni, maarufu kama stesheni kuna shughuli mbalimbali za kibiashara na huduma hufanyika kama vile uuzaji wa chakula, mikeka, matunda, viungo, vocha, maji nk.
Wengi wanakumbuka stesheni maarufu kama vile Kimamba, Kilosa, Saranda Tabora Nguruka, Kazuramimba; kuna biashara za kila aina. Paja au kidali cha kuku wa Saranda wacha mchezo! Asante Rais Samia, umeongeza fursa kwa wananchi wako wa kawaida.
Nne, uhai wa huduma ya treni umeongezeka kwani kulingana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa kwa sasa kutakuwa na safari za treni kwenda Kigoma mara tatu kwa wiki kutoka safari mbili kwa wiki kama ilivyokuwa zamani.
Treni ya kwenda Kigoma kwa safari moja, ina uwezo wa kuchukua abiria 1,500 kwa kutoka Dar es Salaam, ambapo hivi sasa mabehewa yameongezeka kutoka 14 hadi 20 kwa njia ya Kati.
Wakati kwa upande wa Kaskazini treni ya Deluxe itaongeza mabehewa kutoka 6 hadi 16 kwenda mikoa hiyo. Kwa ujumla ndio kusema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameongeza uhai mkubwa kwa Shirika na ameongeza huduma bora ya usafiri kwa wananchi wake.
Fauka ya hayo, Masanja alisema hali hii itaongeza huduma za usafiri na zile presha za abiria au wasiwasi wa kukosa tiketi utaisha, kwani mbali ya mabehewa haya 22 yapo mengine 19 mekundu kwa ajili ya kufanya safari hizo. Hali hii kwa hakika Dkt. Samia anaendelea kuwagusa wananchi wanyonge wa kawaida.
Tano, kuchochea uchumi na kukuza uzalishaji mali. Mabehewa haya yatasaidia kuongeza ari ya uzalishaji kwa wakulima na hata wafanyabiashara. Kuwapo kwa uhakika wa safari za treni ni kujihakikishia kuwapo kwa wateja na hivyo biashara ya uhakika. Hivyo, itaongeza hamu na ari ya kazi kwa wazalishaji. Huu ndio Urais kujali kwa vitendo hali halisi za watu.
Sita, kuongeza kasi ya ushindani wa kibiashara ubora wa mabehewa haya ni ishara ya kuimarika kwa huduma za usafiri wa reli. Bila shaka watoa huduma katika aina nyingine za usafiri zitaimarishwa ili kuhimili vishindo.
Saba, kuchochea ukuaji wa shughuli za utalii huduma ya usafiri wa treni yenyewe tu ni utalii wa kutosha. Kuboreshwa kwa huduma zake sasa kutaongeza idadi ya watalii wengi nao kutumia usafiri huo. Hii inachagizwa na kuwapo kwa vivutio mbalimbali njiani katika treni hiyo.
Watalii watapata fursa ya kushuhudia uoto safi wa asili, mashamba, nyumba za asili, mito, mabonde, ndege, wanyama wawapo njiani. Hakika Mheshimiwa Dkt. Samia amezidi kuinogesha ‘Royal Tour.’
Hali halisi ilivyo ndani ya Treni hii ya Kigoma
Kama alivyowahi kusema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa, kiongozi mahiri hasa akitenda vilivyo, yale mambo mazuri hatayasema yeye bali watayasema wananchi wao wenyewe waliotendewa mambo hayo .
Kauli hii imethibitika jana kwa wananchi hao walipopanda treni hiyo, ambapo kabla ya safari kuanza ilisikika sauti ya mtangazaji ikiwaomba wana dini (Waislamu na Wakristo) kuanza safari kwa sala na dua. Kisha Mtangazaji alitoa matangazo na maelekezo kuhusu treni. Hali hii ilizidi kuwavutia wananchi.
Wengi walituma picha na video kwenye mitandao ya Kijamii wakionyesha mandhari sharifu yaliyomo ndani ya Treni hiyo. Mmoja ya abiria niliyezungumza naye alisema: “treni ni nzuri ina huduma zote kwa kweli bado ni mpya ni nzuri. Kuna maji, feni na sehemu ya kuchaji simu. Kuna muziki na unapata matangazo kwa kila hatua ya safari.”
Abiria mwingine alisema: “Tumefurahi naona na Mkurugenzi mwenyewe yule mweupe tuko naye. Wamepita humu ndani ya Treni wanahimiza usafi na kutuuliza maoni mbalimbali na namna tuiionavyo safari.” Ndio chambilecho Dkt.Samia ukitenda wema watu watasema wenyewe.
Tofauti ya Treni hii na ile ya SGR
Baadhi ya wananchi wametaka kuchanganya katika ya mabehewa haya 22 ya ‘Meter Gauge Railway’ na yale ya mabehewa 14 ya ‘Standard Gauge Railway’ maarufu kama SGR.
Mabehewa ya SGR ni tofauti na haya. Mabehewa ya SGR hayajaanza kazi. Mabehewa haya MGR ni juhudi kubwa za Serikali chini ya Dkt. Samia kuboresha reli ya kati ili iendelee kutoa huduma bora na kuwaondoa wanachi wa kawaida katika hali ya unyonge.
Hata hivyo, pamoja na uboreshaji wa safari za treni kuelekea Kigoma na maeneo mengine, zipo changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi. Kwanza, ni kuna ya kuangalia upya utaratibu wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao, kwani inaonekana tiketi hizo zinaisha mapema, ingawa baadaye wanaonekana baadhi ya watu wakiuza tiketi hizo kwa bei ya juu.
Pili, kwa upande wa wananchi, tuwe mstari wa mbele katika utunzaji wa usafi na vifaa vilivyomo ndani ya mabehewa haya mapya. Tuoneshe uzalendo wa kutunza vya kwetu. Vilevile, maafisa na wafanyakazi wa treni wawe wakali kusimamia mali hizi, lakini wasichoke kukumbusha na kutoa elimu mara kwa mara juu ya umuhimu wa kutunza na kuzingatia matumizi mazuri ya vifaa hivyo.
Sisi abiria wenyewe pia tusiache kukanyana na kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa mabehewa haya. Kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kwa umma, kwani dhamira yake njema ya kuwatumikia Watanzania inazidi kudhihirika kila kukicha.
Ni dhahiri kuwa, kuanza kazi kwa mabehewa haya, pia ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM iliyoahidi kupata vichwa vipya na kuboresha usafiri wa Reli.
Jambo hili pia lilikumbushwa na Kilumbe Shaaban Ng’enda Mbunge wa Kigoma Mjini alipomuomba Dkt. Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani Kigoma la kutaka kuongezeka kwa safari za Treni kwa kuwa usafirishaji huu ndio tegemeo la watu wa kipato cha chini. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelitekeleza hilo kwa vitendo.
Kwa hakika Dkt. Samia ameendelea kuwa sikio la wananchi na kuisimamia Serikali yake. Hili ni jambo muhimu sana. Twamtakia heri na siha tele ili aendelee kuyatenda mema haya kwa Watanzania wenzake.
*Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi Kivukoni Dar es Salaam.