Na Emmaculate Mwalwego, OUT
KADHIA zinazojitokeza mara kwa mara kati ya wanasiasa na vyama vyao vya siasa, vimenisukuma kukumbuka umuhimu wa kuwa na wagombea binafsi.
Ingawa hoja hii iliwahi kutolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani miaka ya nyuma, lakini kwa namna moja ama nyingine, kuna kila sababu ya kutafakari upya na kuangalia uwezekano wa kulifanyia kazi suala hili.
Shabaha kubwa iwe kuondoa sintofahamu inayojitokeza mara kwa mara kati ya wawakilishi wa umma na vyama vyao vya siasa. Kwa mfano, wawakilishi wa umma, wabunge na madiwani mara kadhaa wamejikuta wakilazimika kutii amri za vyama vya siasa kuliko umma uliowachagua.
Wakati fulani wabunge au madiwani wa chama fulani wanaweza kuitwa faragha na kupewa maelekezo au msimamo wa chama chao kuhusu ajenda fulani, kisha wakaingia katika mkutano wa bunge au madiwani na kuja na hoja inayoonekana kuwa na maslahi ya chama kilichowapa dhamana ya uteuzi wao.
Nakumbuka wakati ugonjwa wa COVID-19 ulivyotangazwa rasmi nchini, baadhi ya waliokuwa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliwahi kushinikizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuacha vikao vya Bunge na kwenda kujifungia majumbani kutii agizo la chama, lililowataka kwenda karantini kwa siku 14.
Nakumbuka pia baadhi ya wawakilishi waligomea amri hiyo na kuingia bungeni, baada ya ukaidi huo, Chadema ikatangaza kuwafukuza. Mambo kama hayo yamewahi kujitokeza katika ngazi ya udiwani pia. Vilevile, baadhi ya wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) waliwahi kususia vikao hivyo kutii maagizo ya chama chao.
Hata Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliwahi kufanya hivyo wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba mpya, ambapo wajumbe wa Bunge la Katiba waliwahi kufanya vikao vya pembeni katika kujipanga kutetea maslahi ya CCM kuhusiana na idadi ya serikali mbili. Hata hivyo, ieleweke kwamba, hoja yangu hailengi kuwa na mgombea binafsi katika nafasi ya urais. Mgombea wa urais atokane na chama cha siasa.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba, hoja ya mgombea binafsi siyo ngeni katika siasa za Tanzania. Suala la mgombea binafsi limekuwa likileta mijadala mikali tangu kuanzishwa upya kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa na umechangia katika madai ya mabadiliko ya katiba.
Mchezo wa kujificha unaoonekana katika suala hili unashangaza. Wale wanaotaka kuwepo kwa wagombea binafsi wanakariri vipengele vya katiba vinavyosisitiza haki na wajibu wa raia. Haki hizi ni pamoja na haki ya kupiga kura na kupigiwa kura ambayo haitakiwi kuwekewa mazonge ya vyama vya siasa.
Wale wasiotaka mgombea binafsi awepo, wanadai kuwa ni vigumu kumwajibisha mgombea binafsi hasa kwa masuala ya uwajibikaji. Wanadai kuwa chama cha siasa huweka muundo wa kudhibiti wagombea na hivyo kuwafanya wawajibike zaidi kwa wananchi. Mpaka sasa kuna hukumu tatu za mahakama kuhusiana na suala la mgombea binafsi.
Mwaka 1993 marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, aliyekuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP) alifungua kesi mahakama kuu akitaka mabadiliko katika Ibara za 39 na 67 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwani alidai vinakiuka Katiba.
Uamuzi wa Mahakama, uliosomwa na Jaji Kahwa Lugakingira Oktoba 16, mwaka 1994 ambao unachukuliwa kama ‘hukumu wa kihistoria’. Hukumu hiyo ilikubaliana na mlalamikaji ikitilia mkazo yafuatayo; Mosi, haki za msingi siyo zawadi kutoka kwa dola, isipokuwa zinastahili kutolewa kwa mtu yeyote na zilikuwepo hata kabla ya dola na sheria.
Kuwekwa kwa haki hizo kwenye Katiba ni ushahidi tu wa kuzitambua na nia kwamba, haki hizi zitakuwa na nguvu ya kisheria na haziwezi kuzuiwa bila sababu na dola.
Pili, ibara ya 21(1) inampa haki kila raia kushiriki katika Serikali ya nchi, ama moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa utashi wa wananchi. Haiingiii akilini kwa katiba hiyo hiyo tena katika Ibara ya 20(4) kulazimisha mwananchi kuwa mwananchama wa chama cha siasa ili kugombea.
Tatu, inapotokea kipengele kimoja cha katiba kinapingana na kingine kinachotoa haki ya msingi, mahakama inalazimika kutoa upendeleo kwa haki za msingi na kuacha kipengele kingine ambacho utekelezaji wake huweza kuvunja haki. Ni haki za msingi ambazo mahakama ipo kuzilinda kwa nguvu zote, na siyo vikwazo vya haki.
Badala ya kukata rufaa kupinga uamuzi huu, Serikali iliamua kufuata utaratibu mwingine na kuweka sheria. Ilipofika Desemba 1994 Bunge likapitisha muswada ambao ulikuwa ni mabadiliko ya 11 ya katiba ya mwaka 1994.
Kipengele hiki kiliweka msisitizo kuwa ili Mtanzania agombee uchaguzi katika ngazi yoote sharti awe mwananchama wa chama cha siasa. Suala hili liliibuka tena mwaka 2006 pale Mchungaji Mtikila alipopinga mabadiliko haya ya katiba.
Jopo la majaji wanne walisikiliza kesi hiyo. Hukumu yao ilikuwa kwamba, kuweka vizuizi kwa wananchi kugombea ilikuwa ni kinyume na katiba na uvunjifu wa haki za kidemokrasia zilizopo katika katiba (Gazeti la The Citizen la Jumapili ya Desemba 19, 2010).
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipinga hukumu hii akihoji nguvu ya mahakama kubadilisha katiba. Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ulitolewa na jopo la majaji saba Juni 17 mwaka 2010.
Hukumu hii inafurahisha, kwani haikugusia suala la mgombea binafsi, bali ilijikita katika masuala ya utaratibu na kanuni. Mahakama ilikubaliana na hoja ya Mwanasheria Mkuu kuwa Mahakama haina uwezo wa kubadilisha vifungu vya katiba na kwamba mamlaka hayo yapo kwa Bunge pekee.
Mahakama ilihitimisha hukumu yake kwa kubainisha kuwa suala la mgombea binafisi ni la kisiasa na siyo la kisheria (Gazeti la The Citizen la Desemba 19, 2010).
Mahakama ya Rufaa haikuwa kufikiria kurejea hukumu ya Jaji Lugakingira kuwa mahakama zipo kwa ajili ya kulinda haki za msingi kwa gharama yoyote na siyo kuweka vikwazo. Inashangaza kuwa, Serikali haikufanya chochote baada ya hukumu ya mwaka 2006 na ikasubiri mpaka mwaka 2010 kukata rufaa.
Ni dhahiri kuwa kwa kutoa hukumu mwezi wa Juni 2010, Serikali ilikuwa inapunguza uwezekano wa wanaharakati kupinga tena mahakamani.
Hakika, kuzuia wagombea binafsi ni kinyume cha mwenendo wa siasa za uliberali ambazo Tanzania imeanza kuzifauta mara baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Kwa vyovyote vile, matakwa ya kuwa mwanachama ili kugombea, ni moja ya mabaki ya mfumo wa chama kimoja.
Hili ni eneo ambalo linapaswa kutafakariwa kwa namna moja ama nyingine. Linaweza lisitazamwe katika nafasi ya urais, lakini kwenye nafasi za chini kama vile ubunge, uwakilishi na udiwani linaweza kufanywa.
Maana chama chochote cha siasa kinaweza kumtangaza mtu ambaye siyo chaguo la wananchi, kisha akajitokeza mgombea ambaye ana sifa zote, lakini hana chama, wananchi wakamuunga mkono na akawatumikia.
Kinachoweza kufanywa hapa ni kuwa, kwenye nafasi nyeti kama ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, wagombea wake watokane na vyama vya siasa, lakini uwakilishi mwingine utokane na vyama au mgombea binafsi.
Inaonekana kuwa mgombea binafsi ni mwiba kwa walioko madarakani na hasa chama tawala, na hii inaoonekana kwa jinsi ambavyo suala hili limekuwa likipigwa danadana.