Kuna haja ya kutazama kwa kina Magonjwa yanayotokana na Kung’atwa na Nyoka

0

Na Dkt. Raymond Mgeni

DUNIANI kote hufikia visa Milioni 5.4 vya watu kung’atwa na nyoka (snakebite) huku visa Milioni 1.8 hadi 2.7 ni visa vya kungatwa na nyoka vyenye kuacha sumu (snake envenoming) kwa mtu. Vifo vinavyotokea na kusababishwa na kung’atwa na nyoka kwa mwaka hufikia vifo 140,000 na wakati huo huo kuchangia ulemavu mara tatu zaidi.

Shirika la Afya duniani (WHO) mwaka 2017 iliweka visa vya watu kung’atwa na nyoka kama kundi la magonjwa ya kitropiki yasopewa kipaumbele “Neglected Tropical Disease” na mwaka 2019 shirika la afya likazindua mpango wa kupunguza vifo kufikia nusu ya vifo vinavyotokea kila mwaka na kupunguza maradhi na ulemavu unaoweza kujitokeza kutokana na mtu kung’atwa na nyoka kabla ya kufika mwaka 2030 kwa mipango ya kuihusisha jamii kielimu, kukuza mifumo ya kimatibabu na kuongeza ubia.

Visa vya kung’atwa na nyoka ni suala zito la kiafya la kijamii na la dharura ambalo bado ni tatizo katika ukanda wa kitropiki kwa maeneo mbalimbali Duniani. Ung’atwaji wa mtu na nyoka unaweza kuleta athari kubwa ukiangalia kwa Tanzania kuna karibia spishi (aina) 22 za nyoka ambapo kulingana na “Meserani Snake Park jijini Arusha” inaonesha Tanzania kuna nyoka jamii 4 zenye sumu kali ambapo inajumuisha jamii ya nyoka waitwao Black na Green Mamba, Egyptian Cobra na Puff adder (Kifutu).

Wapo nyoka wenye sumu na wasioacha sumu. Nyoka wenye sumu (venomous snakes) wanaweza kuleta madhara wanapomng’ata mtu ambapo sumu inaweza kuingia kwa mfumo wa damu au misuli. Nchini Tanzania kuna makundi matatu ya sumu zinazozalishwa na nyoka pindi mtu ang’awatapo.

Sumu ya kuleta hitilafu za kimfumo fahamu “neurotoxins’ na kusababisha upoozaji unaoweza kuathiri mifumo kama upumuaji, sumu ya kuharibu tishu za mwili na uvimbaji na tatu sumu ya kusababisha madhara kwenye chembe sahani na uharibifu wa tishu za damu “hematoxins”. Madhara ya sumu haya yanaweza kusababisha vifo na ulemavu kwa watu.

Waathirika wakubwa wa kung’atwa na nyoka ni watu ambao wanajishughulisha na kilimo, wawindaji, wavuvi, wanafanya kazi maeneo yenye wingi wa misitu na kundi la watoto ambao hucheza sehemu zenye vichaka au maporini.

Madhara makubwa ya ung’atwaji na nyoka huonekana katika uharibifu wa tishu za mfumo wa misuli na mifupa ambapo kumesababisha ukatwaji wa mikono na miguu endapo athiriko ni kubwa na mtu alicheleweshwa kufika hospitalini. Karibu visa zaidi ya 43,000 kwa mwaka huripotiwa vya watu kungatwa na nyoka Afrika.

Tanzania ni nchi ambayo haina utoshelevu mkubwa wa utafiti wa visa vya watu kung’atwa na nyoka, namna ya kufuata matibabu bado matibabu mengi yanafanyika kijadi.

Ingawa matibabu ya mtu aking’atwa na nyoka yana changamoto kutoka ngazi ya jamii hadi ngazi ya hospitali. Matibabu ya mtu aliyeng’atwa na nyoka ni matumizi ya dawa ya kuua sumu ya nyoka itengenezwayo kutoka kwa sumu ya nyoka iitwayo “anti-venom”. Hii ndiyo tiba bora pekee ya kuumwa na nyoka ingawa si rahisi kupatikana.

Ila si hivyo hutokea pindi watu wanapong’atwa na nyoka, wengi hukimbilia matibabu ya kijadi kwanza au kuambiwa funga juu ya eneo mtu alipong’atwa bila utaalamu ambacho ni kitendo rahisi kunyima mtiririko mzuri wa damu unaoweza kuleta shida kwenye eneo na kuharibu baadhi ya tishu za mwili.

Kuna kisa cha mtoto mmoja alikuja hospitali akiwa na kidonda kibaya kilichopelekea kukatwa mkono (amputation) wake wa kulia kuanzia kiwiko kilichotokana na kung’atwa na nyoka wiki mbili zikiwa zimepita bila kupatiwa matibabu ya hospitali. Hiki ni kisa kimoja tu, kuna visa vingapi ambavyo watoto ambao ndio waathirika wakubwa wanatibiwa kienyeji?

Elimu ya namna msaada wa haraka kwa mtu aliyeng’atwa na nyoka inahitajika ili kuepusha ulemavu ambao hujitokeza katika visa vingi kwa sababu ya kuchelewa kumhudumia muhanga wa kung’atwa huku wakiamini katika njia za jadi ambazo wakati mwingine ujuzi ni mdogo. Wakati mwingine wanaong’atwa na nyoka huachwa na vidonda hivyo vinaposhindwa kutibiwa kwa njia salama ni rahisi vidonda hivi kupata maambukizi ya kibakteria na kusababisha madhara makubwa zaidi.

Ingawa zipo juhudi zinazoendelea nchini Tanzania mfano Neema Lugangira (Mb) ambaye ni Balozi wa magonjwa ya Kitropiki yasiyopewa kipaumbele kupitia mitandao ya kijamii kuweza kushiriki katika majadiliano na Dkt. George Kabona (Meneja wa Kitaifa wa mradi wa kupambana na magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya) ni jitihada kubwa za kuungwa mkono katika kuisaidia Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mradi mkubwa wa ‘snakebites’ ambao uko mbioni kuanzishwa katika nchi za Afrika.

raymondpoet@yahoo.com
0676 559 211

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here