Wajawazito na changamoto ya afya ya akili

0

Na Dkt. Raymond Mgeni

AFYA ya akili kwa mama mjamzito ni muhimu sana, kutokana na ukweli kuwa, kipindi cha ujauzito ni chenye mkazo mkubwa, ambapo muhusika anakutana na mabadiliko ya kimwili, kiakili na kihisia.

Ujauzito unaleta mabadiliko ya kiakili kwa mama mjamzito, ambapo kunahitaji ukaribu wa kuhakikisha kipindi hiki, anasaidiwa kukabiliana na mabadiliko mbalimbali.

Magonjwa ya akili kwa akina mama wajawazito na wanaojifungua huenda hayatazamwi kwa ukubwa na jamii, ila yanajitokeza na kuathiri na kuwa na maendeleo yasiyo mazuri kimatibabu.

Shida kubwa ni Sonona kipindi cha ujauzito; baada ya kujifungua na hali ya kupata kichaa baada ya kujifungua. Hali hizi zinachangia matatizo yajulikanayo ya magonjwa na changamoto ya akili kwa mama wajawazito na baada ya kujifungua.

Tafiti zinaonesha, wanawake wawili kati ya idadi ya wanawake 1,000 wanaokuwa wamepata ujauzito hadi kujifungua, wanapata changamoto za Sonona na hali ya ugonjwa wa akili kunakochangiwa na sababu nyingi.

Sababu ya uwepo wa matatizo ya magonjwa ya akili yaweza kuhusishwa na magonjwa ya kurithi ya kifamilia, matumizi ya vilevi, hali ya kimsongo wa mawazo endelevu, magonjwa ya ndani sugu na sababu za ushindwaji kukabiliana na matukio kama kufiwa, kukataliwa hususani mimba iliyokataliwa.

Kwa ujumla wa hizi sababu zinaweza kuwa moja ya kiini kinachosababisha hali mbaya kiakili kwa mama mjamzito. Duniani kote afya ya mama na mtoto inapewa kipaumbele kikubwa na ipo katika malengo makubwa ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya hadi 2030.

Umuhimu wa kujali afya ya mama na mtoto ni maandalizi ya kujenga jamii bora na yenye kuepusha utegemezi wa matatizo mengi yanayoweza kujitokeza kwa mama au mtoto.

Kuna kundi la akinamama wajawazito ambao wanapata tatizo la kuugua akili wakiwa wajawazito; na kundi la pili ni wale ambao wamepata ujauzito huku ni wagonjwa wa akili tayari; na kundi la tatu ni wale ambao wanapata changamoto za akili, pindi muda mfupi wa siku 42 toka wameshajifungua.

Wapo ambao wanapata matatizo ya Sonona wakishakuwa wamepata watoto, na wengine kupata kabisa changamoto za kiakili kunakohitaji matibabu ya kulazwa, kuepusha hali hatarishi wanayoweza kuifanya dhidi yao wenyewe na watoto.

Vimekuwepo visa vingi ambavyo pindi mama aliyekuwa mjamzito akishajifungua kukutana na hali za changamoto ya uuguaji wa akili unaoweza kuambatana na dalili za mtu kupoteza uhalisia, tabia za ukali, hali ya kuona mtoto aliyejifungua ni tishio kwake na hata wengine kufikia kuhatarisha maisha ya mtoto kama kumtupa mtoto, kufukia mtoto au kuua kabisa.

Yote haya yanachangiwa pale ambapo mama amepata changamoto ya akili za kupoteza uhalisia, udumavu wa kufikiri, kumbukumbu na kutojitambua kwa akifanyacho. Suala hili linahitajika sana kuangaziwa jicho la tatu pindi mama aliye mjamzito kuangaliwa na kusaidiwa pindi anapopata changamoto za kiakili.

Si hilo tu, hali ya Sonona inaweza kumfika mama mjamzito endapo kipindi cha ujauzito aliambatana na mkazo mkubwa. Mkazo unaweza kuwa ujauzito uliokataliwa, hali duni ya kimaisha, ujauzito kipindi cha masomo au ujauzito wenye kuambatana na maambukizi mbalimbali ya magonjwa. Mama mjamzito anayepata changamoto za masuala ya kiakili anahitaji maangalizi makubwa dhidi ya hali yake kiafya.

Kusaidiwa juu ya mahudhurio ya kliniki, maangalizi ya ukuaji wa mtoto tumboni na kuwa tayari kubaini hali zozote za hatari zinazoweza kujitokeza kipindi cha ujauzito. Kukosekana kwa ukaribu wa wanafamilia au huduma za kimatibabu kwa kundi hili kuna hatari kubwa juu ya mahudhurio mabaya ya kliniki kipindi cha ujauzito.

Mama aliyepata changamoto za kiakili na hajapata matibabu ni ngumu sana kuwajibika kwa malezi ya mtoto aliyezaliwa hata kufikia wakati mwingine udumavu kwa watoto ambao wanazaliwa endapo ndugu wa karibu hawatawajibika kwa niaba.

Siku za mwanzo toka mtoto amezaliwa anahitaji uangalifu katika kunyonyeshwa, kugundua mabadiliko yoyote na hata mahudhurio ya chanjo. Pasipokuwepo na msaada wa karibu kuna hatari ya udumavu kwa mtoto, utapiamlo kunakoathiri maisha ya mtoto na kifo.

Jamii hujikuta na dhania potofu kuyaona haya mabadiliko anayopata mama mjamzito, mama aliyejifungua au anayenyonyesha, kukutana na changamoto za akili, kusema ni kulogwa au kuchezewa; mbali na kutokujua hali hizi zinajitokeza kwa sababu mbalimbali, zikiwepo mkazo mkubwa au msongo mkubwa wa mawazo, unaokuja kipindi cha ujauzito na kukutana na migogoro mbalimbali ya kifamilia.

Tatizo hili limechangia kwa wengi kutengwa, au pengine kuachwa kabisa pindi wanapopata hizi changamoto. Hili ni eneo muhimu kuendelea kutoa elimu dhidi ya hizi shida za kiakili, Sonona kwa mama aliyejifungua kusaidika.

Matibabu hutolewa katika hospitali hususani zile zenye nafasi ya kuwaona watu wa magonjwa ya akili. Matibabu dawa na matibabu ya kisaikolojia yanasaidia sana kuwawezesha kutibu akili na mama kuweza kuwajibika na hali ya uleaji mtoto, kubeba mimba hadi kujifungua na uonyeshaji.

*Mwandishi wa makala hii ni Mtaalam wa afya katika Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya, Idara ya Magonjwa ya Akili. Kama una maoni, maswali au ushauri, anapatikana kwa Barua pepe raymondpoet@yahoo.com, au simu namba +255 676 559 211.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here