Na Mohamed Saif
WAZAWA na Wadau wa maendeleo ya Kata ya Lupila Wilayani Makete Mkoani Njombe wamechangia kiasi cha Shilingi Milioni 20.8 kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Sekondari ya Lupila.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 31 ya Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Lupila amebainisha hayo Oktoba 15, 2022 kwa niaba ya wadau hao.
“Wadau kwa umoja wetu, tumechanga kiasi cha Shilingi Milioni 20,810,000 na tumezitolea maelekezo makhsusi fedha hizi ambapo kiasi cha Shilingi 17,700,000 kipelekwe kwenye kuboresha miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na vitanda na madawati kwa ajili ya wanafunzi wetu,” alisema Mhandisi Sanga.
Aidha, kiasi cha fedha kilichobaki kilikabidhiwa kwa wanafunzi waliofanya vizuri (wahitimu kidato cha sita waliopata daraja la kwanza kwa alama saba hadi tisa) sambamba na walimu ikiwa ni motisha kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Alisema, wanafanya hayo ili kuwapunguzia mzigo wazazi lakini pia kusaidiana na Serikali hasa ikizingatiwa kuwa Serikali inalo jukumu hilo kwa nchi nzima.
“Tunaamini Serikali hili ni jukumu lake la msingi na inafanya hivi nchi nzima lakini pale ambapo wadau tunaona tunaweza kuchangia basi hapa ndipo nasi tunapoweka mkono wetu,” alifafanua Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alipongeza jitihada za walimu na wanafunzi wa Sekondari ya Lupila ambazo alisema zinawahamasisha wadau kuendelea kuichangia shule hiyo ili ifike mbali zaidi.
Alisema, matokeo ya Kidato cha Sita yamekuwa ya kivutio cha kipekee hasa ikizingatiwa kuwa licha ya shule hiyo kutoa watahiniwa wa kidato cha sita kwa mara ya kwanza hapo mwaka jana, lakini walifanikiwa kuongoza kimkoa kwa kushika nafasi ya kwanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Lupila, Yohana Madope ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mahafali hayo alipongeza jitihada binafsi za Mhandisi Anthony Sanga katika kushirikiana na wananchi wake kwenye shughuli za kimaendeleo na kijamii.
“Mhandisi Sanga wananchi wa Lupila tunakushukuru sana, matendo yako ni ya kipekee haijawahi kutokea, tunaendelea kukuombea unafanya mambo makubwa nyumbani kwako usichoke, ninakuomba wewe na wadau wengine muendelee kutusaidia kuijenga Lupila yetu na tunawasihi muendelee kuhamasisha na wengine,” alisema Madope.
Naye Diwani wa Kata ya Lupila, Ernesta Lwila alipongeza jitihada za wadau hao kwenye kuinua suala la elimu hata hivyo aliwasihi wajikite pia kwenye masuala mengine ili kuinua uchumi wa Lupila.
Akizungumzia kwa ujumla uratibu, dhamira na umoja wa wadau hao, Katibu wa wadau Aliten Ntullo ambaye pia ni mwalimu wa Sekondari ya Njombe alisema, wameunda kundi sogozi ambalo linashirikisha wazawa wa Lupila waliopo nje na ndani lengo likiwa ni kujadili na kuhamasisha maendeleo.