‘Mwarobaini’ wa kukomesha vitendo viovu watajwa

0

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Misikiti pamoja na Madrasa zinazojengwa zinapaswa kutumika kuielimisha jamii umuhimu wa malezi bora ya watoto ili wawe na khofu ya Mungu.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema hayo, katika ufunguzi wa Msikiti mpya wa Al hudda uliopo eneo la Masingini Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja, uliojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya ‘Al-noor Cheritabla Agency for the Needy’, hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alisema, kumekuwepo mmong’onyoko mkubwa wa maadili katika jamii hususan kwa vijana kujihusisha na vitendo viovu, ikiwemo vya Udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na Wizi na ubadhirifu wa mali za Serikali, mambo aliyoeleza yanapaswa kuzungumzwa na kupatiwa ufumbuzi kupitia Misikiti.

Alisema, matukio hayo na mengineyo mengi yaliyo kinyume na maadili yamekuwa yakifanyika kwa vile jamii imekosa khofu ya Mungu, hivyo akatoa rai kwa jamii kuimarisha malezi mema kwa watoto tangu wangali wadogo ili waweze kukua wakiwa na khofu ya Mungu.

Katika hatua nyingine, Alhaj Dkt. Mwinyi aliutaka uongozi kusimamia utunzaji wa msikiti huo ili waumini wanaofika waweze kutekeleza ibada katika mazingira bora.

Aliwapongeza wafadhili waliojenga msikiti huo pamoja na wananchi wote waliofanikisha ujenzi huo na akatumia fursa hiyo kuwashukuru kwa dhati kwa kujenga eneo la kuchezea watoto, akibainisha hatua hiyo itatoa fursa kwao ya kucheza pamoja na kujifunza.

Aidha, aliipongeza taasisi ya Al –Noor Cheritable Agency for the Needy kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuenga majengo mbali mbali ya kidini pamoja na Huduma za kijamii katika ameneo mbali mbali nchini.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaab alisema hatua ya Rais Alhaj Dkt. Mwinyi ya kufungua msikiti huo ni kitendo kitukufu kilichopata kufanywa na Mtume Muhammad (SAW).

Mapema, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali mfaume aliwataka waislamu kuuimarisha msikiti huo kwa kuunadhifisha na kuufanyia matengenezo pale unapoharibika, sambamba na kutumika kama kituo cha kupata taaluma.

Sheikh Khalid aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kuwatupia lawama Viongozi kwa mambo maovu yanayofanyika katika jamii na akatumia fursa hiyo kuitaka jamii kufanya juhudi kuyaondoa maovu hayo kwa mikono yao.

Alisema, katika zama hizi mitandao imekuwa ikitumika vibaya kubadili mitazamo ya mambo mema ili yaonekane mabaya na hayana manufaa yoyote kwa jamii, akitolea mfano suala la Utalii, ambapo ndani ya Kuraani limebainishwa kuwa na manufaa.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa ‘Al-noor Cheritable Agency for the Needy ‘ Sheikh Nadir Mahafoudh aliushukuru uongozi wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) kwa kusaidia upatikanaji wa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo pamoja na ujenzi wa ukuta.

Alisema, Taasisi hiyo imekubali ombi la la wananchi na Uongozi wa kikosdi hicho cha KMKM la kujenga Kiliniki katika eneo hilo, ili kuwandolea shida ya matibabu inayowakabili.

Alisema, msikiti huo una uwezo wa kuswaliwa na waumini 700 kwa wakati mmoja kupitia eneo la ndani na nje, huku wanafunzi wapatao 250 wataweza kupata fursa ya kujifunza katika madrasa hiyo.

Aidha, Khatibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Abdulkarim Said alisisitiza umuhimu wa waislamu kufanya juhudi na kiujenga, kujikurubisha, kuipenda na kujishughulisha na masula mbali mbali yanayohusu msiikiti, kwa kigezo cha kupata fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here