Na Charles Charles
LILE linaloitwa ni ‘bao la mkono wa Mungu’ ambalo lilifuatiwa na ‘bao la karne’, yameacha kumbukumbu ya kudumu kwa mashabiki wa soka sehemu zote duniani. Ilikuwa ni mechi ya robo fainali za Kombe la Dunia iliyozikutanisha timu za Taifa za Uingereza na Argentina na kuchezwa kwenye Uwanja wa Azteca mjini Mexico City, Mexico Juni 22, 1986.
Ilizikutanisha nchi mbili pia zilizokuwa zimepigana vita vya kuvigombea visiwa vya Falklands vilivyopo Amerika Kusini mwaka 1981, vile ambavyo bado vilikuwa katika kumbukumbu ‘mbichi’ vichwani mwa wananchi wake. Mbali na vita hivyo, mechi hiyo katika upande mwingine iliibua kumbukumbu za mbali zaidi za pambano jingine la Kombe la Dunia lililozikutanisha kwenye Uwanja wa Wembley jijini London, Uingereza mwaka 1966.
Tokea kipindi hicho hadi leo, mechi za kandanda kati ya Uingereza na Argentina zimekuwa na kila aina ya kuhasimiana, mvutano, kukamiana na hata vinginevyo ambapo zinapokutana husababisha kiwewe kikubwa kwa mashabiki wa nchi hizo mbili.
Hata hivyo, mbali ya yote ikiwemo pambano hilo kuonekana muhimu kwa kila upande, aliyekuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina, Diego Armando Maradona (marehemu) ndiye aliyeleta na kuacha gumzo la kudumu duniani kote kupitia mechi hiyo moja peke yake.
Argentina iliingia katika dimba la Azteca huku ikijiamini zaidi kuliko Uingereza. Ikiongozwa na Maradona aliyeonekana kuwa ni mwanasoka mahiri zaidi duniani wakati huo, timu hiyo ilisafiri kutoka nyumbani huku ikiwa na dhamira moja tu kubwa; kwenda Mexico na kushinda Kombe la Dunia.
Sifa kubwa ilizopata Uingereza wakati wa fainali za michuano kama hiyo za mwaka 1966 iliyofanyika katika ardhi yake yenyewe, zilikaribia kujirudia tena kutokana na jinsi ilivyokuwa imeanza vizuri pia huko Mexico mwaka huo wa 1986.
Gary Lineker ambaye ndiye aliyekuwa mshambuliaji wake hatari zaidi akisaidiwa na Peter Beardsley, alianza kwa kuonyesha umahiri mkubwa alipoweza kuitungua Poland kwa “hat-trick”, kisha akaisambaratisha pia Paraguay kwa mabao yake mawili katika mechi ya pili kwa Waingereza.
Lakini, kutokana na kutokuwa uwanjani siku hiyo kwa majeruhi Bryan Robson, kufungiwa kwa Ray Wilkins na nafasi yake kuchukuliwa na Bobby Robson kwa hakika kulionekana ni pengo.
Ingawa mlinzi wa Uingereza, Terry Fenwick alifanya shambulizi kali la mapema zaidi katika lango la Argentina, vijana hao kutoka Amerika Kusini walijibu kwa haraka pia katika dakika ya nane.
Dakika tano baadaye, Maradona alifanikiwa kuipangua ngome ya Uingereza na kuwekwa chini na Fenwick umbali wa mita 25 kutoka golini, lakini mpira wa adhabu alioupiga yeye mwenyewe uliokolewa kwa ufundi mkubwa na kipa mkongwe na mzoefu wa mabingwa hao wa Kombe la Dunia kwa mwaka 1966, Peter Shilton.
Shambulizi hilo lilijibiwa hima na Uingereza dakika moja baadaye wakati kiungo mchezeshaji, Glenn Hoddle alipowapenya mabeki wa Argentina, lakini shuti lake kali likadakwa na kutemwa na kipa Nery Pumpido na mpira huo kumkuta Peter Beardsley, lakini kiki yake naye ikaishia kugonga pembeni mwa nyavu za goli.
Kuanzia hapo, Carlos Bilardo akaanza kumchezesha vyema Maradona ambaye naye alianza kuonyesha ni namna gani alikuwa ni mchezaji wa aina yake duniani.
Alianza kuwatesa kwa chenga za maudhi mabeki wa Uingereza, akatengeneza mipira kadhaa ya adhabu nje ya ‘box’ kutokana na kuchezewa rafu za kibabe, zile ambazo moja kati yake ilikuwa nusura aipatie bao la kuongoza katika dakika ya 33 alipopiga ‘frii kiki’ ya kutoka umbali wa mita 25 na kuokolewa na kipa Shilton.
Lakini, kuanzia hapo Argentina ikawa ni mwiba mkali, mara kadhaa kikosi chake cha mbele kikionyesha kuusumbua kwa kiasi kikubwa ukuta wa timu ya taifa ya Uingereza. Mfano katika dakika ya 40, aliyekuwa beki kisiki wa timu hiyo, Butcher alikabiliana uso kwa uso na Maradona, lakini kama mlinzi huyo kutoka mji wa Ipswich alidhani angeweza kumdhibiti alikuwa amekosea sana.
Shujaa huyo alionyesha umahiri mkubwa kwa kuruka kiunzi cha beki huyo, kisha akarudi na kumpiga “tobo” kwa jinsi iliyoonekana kamwe isingewezekana, lakini ikawezekana! Uhondo mwingine mkubwa katika lango la Uingereza ulitokana na shambulizi la kushtukiza lililofanywa na Jorge Valdano, lakini kiki yake ikagonga mwamba na kurudi uwanjani na mpira huo ukamwendea Steve Hodge ‘aliyeosha’
kwa juu.
Hatimaye ilipofika dakika ya sita ya kipindi cha pili cha mchezo huo, Diego Armando Maradona alirejea kwa nguvu katika lango la Uingereza na kufanya ‘vitu vyake’ kwa kumzidi ujanja golikipa Peter Shilton. Katika kuwania mpira ule wa juu wote kwa pamoja waliruka hewani, lakini Maradona akaupiga kwa mkono wake wa kushoto na kutumbukia wavuni kuiandikia timu yake bao la kuongoza.
Kutokana na hali hiyo, mwamuzi Ali Bennaceur wa Tunisia alizongwa na wachezaji wa Uingereza wakipinga bao hilo wakati tayari akiwa amelikubali na kuelekeza mpira uwekwe katikati ya dimba hilo la Azteca, lakini kamwe hakubadili uamuzi huo.
Maradona mwenyewe aliyekuja kuliita kuwa ni ‘bao la mkono wa Mungu’ wakati mechi hiyo ya kihistoria ilipokuja kumalizika, alionyesha maajabu kwa kusahihisha kile kilichokuwa kimetokea na kuandika bao ambalo hadi leo linaitwa kuwa ni ‘bao la karne’.
Ilikuwa ni dakika ya 55 alipopokea mpira akiwa ndani ya nusu ya eneo la upande wa timu yake mwenyewe, akawapiga chenga Peter Beardsley na Peter Reid, kisha akaanza kumpangua kila mchezaji wa Uingereza aliyekuja mbele yake na kufikia jumla yao saba, halafu akahitimisha kwa kumtungua golikipa Peter Shilton akiwa ni wa nane katika orodha hiyo.
Mbele ya mashabiki 115,000 waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Azteca, Maradona aliyekuwa akiwapangua wachezaji hao jinsi anavyotaka yeye mwenyewe, alifunga bao hilo la pili kwake na timu yake pia kwa udhalilishaji mkubwa dhidi ya kipa Shilton.
Lilikuwa ni bao la aina yake duniani na kutoka kwa mwanasoka mwenye kipaji cha aina yake pia. Lilikuwa ni bao lililopelekea baadhi ya makocha waliokuwa uwanjani wavichanechane vitabu vya kufundishia soka kwa kuviona kuwa vya uongo.
Hawakutaka kuviamini tena kwa vile wachezaji wote saba wa ndani wa Uingereza na kipa wao kila mmoja alimkabili kwa kufuata kikamilifu uchezaji wa soka ambalo wamefundishwa kwa kutumia vitabu, lakini yeye alikuwa akipita kwa jinsi atakavyo kuanzia mwanzo hadi kwa kipa Shilton.
Pamoja na Uingereza kujipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 78 lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji tegemeo wa Everton, Gary Lineker na kuwa la sita kwake katika fainali hizo za Kombe la Dunia nchini Mexico, lakini hadi kilipopigwa kipenga cha mwisho Argentina ndiyo iliyotoka kifua mbele kwa ushindi huo wa mabao 2 – 1.
Ulikuwa ushindi wa mabao hayo mawili ya Maradona uliing’oa Uingereza katika fainali hizo, huku Argentina kwa upande wake ikitinga nusu fainali, kisha kuanzia hapo akasababisha nchi hizo mbili maarufu kwa kandanda duniani ziwe na uadui wa kudumu.
Diego Armando Maradona alifariki dunia Novemba 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 60. Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari duniani, Maradona alifanyiwa upasuaji wa ubongo mapema mwezi huu, huku madaktari wakithibitisha kuwa alifaulu upasuaji huo na huenda wangeanza kushughulikia tatizo lililokuwa likimsumbua la uraibu wa pombe.
Katika maisha yake ya soka Maradona amevitumikia vilabu mbalimbali duniani akiwa kama mchezaji na kocha baada ya kustaafu soka mwaka 1997 alipokuwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake (miaka 37) katika klabu ya Boca Juniors.
Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Argentina, lakini alibwaga manyanga baada ya kipigo cha mabao (4-0) dhidi ya Ujerumani kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 yaliyofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika (Afrika Kusini).
Hadi mauti yanamkuta, Maradona alikuwa kocha wa Gimnasia de La Plata inayoshiriki ligi kuu nchini Argentina baada ya kuachana na vilabu alivyopita katika Mataifa ya Falme za Kiarabu pamoja na Mexico.