Na Happyness Hans, WAF – Mbeya
ZAIDI ya wagonjwa 500 wenye magonjwa ya saratani wamepata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), inayotoa huduma kwa wakazi kutoka mikoa saba ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi.
Akizungumza Septemba 15, 2026 wakati wa kupokea msaada wa dawa na vifaa tiba kutoka Jema Foundation, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Saratani cha Hospitali hiyo, Dkt. Tibera Rugambwa, amesema idadi hiyo inaonesha ukubwa wa changamoto ya saratani katika eneo hilo.
Dkt.Rugambwa amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi na kufika katika vituo vya afya mapema wanapobaini dalili, ili kupata matibabu kwa wakati na kuongeza nafasi ya kupona.
Aidha, Dkt. Rugambwa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuimarisha huduma za saratani nchini, akieleza kuwa kuanzishwa kwa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kumewezesha wananchi kupata matibabu karibu na maeneo yao wanayoishi, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo baadhi ya huduma zilikuwa zinapatikana katika vituo vichache nje ya Kanda wanazoishi Wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jema Foundation, Jema Baruani, amesema msaada huo umetolewa kwa lengo la kuwapa wagonjwa moyo na matumaini katika kipindi cha matibabu pia ni mmoja wa manusura wa saratani ya Hodgkin’s Lymphoma baada ya kuishi na ugonjwa huo kwa miaka tisa, amewataka wagonjwa kutokata tamaa na jamii kuachana na imani potofu zinazoweza kuwafanya kuchelewa kupata huduma za kitabibu.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja Jema Foundation kusaidia wagonjwa wenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Awesu Mchepange, amemshukuru Jema Foundation na wadau wengine kwa kuunga mkono huduma za saratani.
Amesema upatikanaji wa huduma katika hospitali hiyo umesaidia kupunguza gharama na changamoto za wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu, huku akiwahimiza wadau zaidi kujitokeza kusaidia hospitali na wagonjwa wenye uwezo mdogo wa kugharamia matibabu.
Naye Mwakilishi wa Silent Ocean katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati, Gilbert Nyangwe, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Jema Foundation katika kuunga mkono huduma za afya.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa Jema Baruani kuwatembelea wagonjwa wa saratani hospitalini hapo na kuwapatia zawadi pamoja na ujumbe wa matumaini, huku akiwasisitiza kuwa saratani inatibika na wagonjwa wanapaswa kuendelea kuwa na matumaini katika safari yao ya matibabu.