Na Albert Kawogo
KWA mujibu wa takwimu za hivi karibuni za serikali, Mkoa wa Kigoma una ukubwa wa eneo: takribani Kilomita za mraba 37,040, ukiwa miongoni mwa mikoa mikubwa nchini, huku idadi ya watu ikifikia 2,470,967(Sensa ya Watu na Makazi 2022).
Kwa takwimu za Benki kuu ya Tanzania za mwaka 2024 zimeonyesha kuwa pato la Mkoa (GDP) linafikia takribani Shilingi Trillioni 5.6 na pato la wastani kwa mtu (GDP per capita): ni Shilingi Milioni 2.16.
Nguzo kuu za uchumi wa Kigoma zinatajwa kuwa ni Kilimo cha mazao kama michikichi, kahawa, muhogo, mahindi na maharage).
Shughuli nyingine za kiuchumi ni uvuvi katika Ziwa Tanganyika pamoja na biashara ya mipakani ( DRC na Burundi)
Pia, kuna shughuli za uchimbaji wa madini katika baadhi ya maeneo nausafirishaji kupitia Bandari ya Kigoma.
Kwa kuzingatia eneo lake, idadi ya watu na nafasi yake ya kijiografia, Kigoma ina uwezo mkubwa wa kukua na kuwa kitovu muhimu cha biashara kwa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu endapo uwekezaji katika reli bandari na viwanda utaendelea.
Wataalam mbalimbali wa uchumi na biashara za uwekezaji wanaamini kuwa kama nguvu kubwa inayotumika katika kuiistawisha Kigoma kwenye maeneo ya miundombinu ya reli na bandari itaendelea.
Kati ya mwaka 2030 hadi 2050 Kigoma inaweza kuwa miongoni mwa miji yenye nguvu kubwa kiuchumi kuliko mkoa wowote nchini Tanzania.
Ndoto hii itatimia endapo miradi ya SGR, usafiri wa anga, usafiri wa majini na maendeleo ya bandari itatekelezwa kikamilifu na Serikali.
Ziko sababu ambazo zinaweza kusababisha mabadiliko haya kwa haraka na mojawapo ni kwamba, Kigoma ni mlango wa soko la watu zaidi ya Milioni 150 hapa ifahamike kuwa
kwa miaka mingi, Dar es Salaam imekuwa lango kuu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki kama Uganda, Rwanda na Burundi, zenye idadi kubwa ya watu, hivyo kwa kuunganishwa na reli ya SGR, Kigoma ina nafasi ya kuwa kitovu kikubwa cha biashara kinachounganisha Tanzania na nchi za Afrika ya Kati na Kusini, hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi ambazo kwa pamoja zina soko la watu zaidi ya Milioni 150.
DRC ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini, misitu na mazao mbalimbali. Endapo miundombinu ya reli, bandari na usafiri wa majini itaimarishwa, Kigoma inaweza kuwa mojawapo ya njia muhimu za kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda DRC kupitia Ziwa Tanganyika.
Sababu nyingine ni gharama nafuu za uzalishaji na fursa za viwanda. Dar es Salaam imeendelea kukua kwa kasi, jambo ambalo limeongeza gharama za ardhi, usafiri na uendeshaji wa biashara.
Kigoma bado ina nafasi kubwa ya ardhi na gharama zinazoweza kuwa nafuu kwa wawekezaji. Hali hiyo inaweza kuvutia ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao, samaki, madini na bidhaa nyingine zinazotoka ukanda wa Magharibi na nchi jirani.
Iwapo hili litatimia, ajira, mapato ya wananchi na ukusanyaji wa kodi vinaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Pia, tofauti na miji mingine iliyojaa tayari, Kigoma bado ina eneo kubwa la kuendelezwa kwa mipango ya kisasa ya miji, viwanda na huduma za usafiri.
Ikiwa itaunganishwa kikamilifu na reli ya kisasa ya SGR, bandari zilizoboreshwa, usafiri wa anga na miundombinu mingine, inaweza kujengwa kama kitovu kipya cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Magharibi.
Mfano unaotajwa mara nyingi ni mabadiliko ya miji kama Shenzhen nchini China, ambayo ilikua kwa kasi baada ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na sera za uchumi.
Miradi Inayoweza Kubadilisha Kigoma
Uboreshaji wa bandari na ongezeko la meli za mizigo katika Ziwa Tanganyika. Reli ya Kisasa ya SGR (Tabora–Kigoma), ambayo inatarajiwa kupunguza muda na gharama za usafirishaji.
Ujenzi na uboreshaji wa magati ya mizigo na abiria ili kuongeza uwezo wa bandari.
Miradi hii inaweza kuiunganisha Kigoma kwa ufanisi zaidi na masoko ya ndani na ya nchi jirani.
Mwisho, Dar es Salaam itaendelea kuwa kitovu muhimu cha fedha, biashara na huduma nyingine muhimu. Hata hivyo, endapo uwekezaji wa miundombinu, viwanda na biashara utaendelea kama ilivyopangwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Kigoma ina nafasi ya kujitokeza kama moja ya vituo vikubwa vya biashara, usafirishaji na uchakataji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Safari hiyo haitakuwa rahisi, lakini kwa mipango sahihi na uwekezaji endelevu, ndoto ya Kigoma kuwa kitovu kikubwa cha uchumi inaweza kuwa karibu na uhalisia.