Na Shaban Juma, Accra, Ghana
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutambulika kimataifa kama Champion wa Umoja wa Afrika (AU) katika juhudi za kuharakisha kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama, akiongoza mjadala wa kisiasa kuhusu utekelezaji wa Ramani ya AU ya mwaka 2030 wakati wa Kikao Maalum cha Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kilichofanyika jijini Accra, Ghana.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Rais amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kuongeza dhamira ya kisiasa ili kuhakikisha Afrika inafikia malengo ya kutokomeza UKIMWI, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Samia amesema Tanzania imeunganisha utekelezaji wa Ramani ya AU ya mwaka 2030 katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2026/2027–2030/2031, huku ikiendelea kuwekeza katika huduma za afya msingi, afya ya mama na mtoto, pamoja na kuimarisha huduma za kinga na tiba nchini.
Ameeleza kuwa mafanikio ya Tanzania katika kupunguza vifo vya akina mama yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na matumizi ya mfumo wa kidijitali wa rufaa za dharura wa m-Mama, hatua zinazolenga kufikisha kiwango cha vifo vya akina mama chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Kwa nafasi yake kama Champion wa Umoja wa Afrika katika eneo hilo, Rais ametoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kuimarisha ushirikiano, kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya na kutekeleza kwa vitendo Ramani ya AU ya mwaka 2030 ili kujenga mifumo imara ya afya na kuhakikisha kila Mwafrika anapata huduma bora za afya.