WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali inalenga kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaenda sambamba na ongezeko la ajira na kipato kwa wananchi.
Mkumbo amesema hayo alipofungua Wiki ya Ubunifu Tanzania 2026, iliyoandaliwa kwa ushirikiano baina ya Tume ya Taifa ya Mipango na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, pamoja na wadau wengine jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, utekelezaji wa Dira 2050 hautapimwa kwa takwimu za ukuaji wa uchumi pekee, bali kwa uwezo wa uchumi huo kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
“Uchumi hauwezi kukua kwenye takwimu peke, lazima ukuwe kwenye mifuko ya wananchi wetu. Ukuaji wa uchumi unaonekana pale ambapo wananchi wanapata kipato zaidi kupitia ajira au biashara,” amesema,
Awali Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Tausi Mbaga Kida, alieleza muktadha wa tukio hilo kuwa linafanyika katika kipindi muhimu cha utekelezaji wa Dira 2050, inayolenga kuweka msingi wa ujenzi wa Tanzania yenye maendeleo jumuishi na endelevu.
“Mawazo bunifu yanahitaji kuunganishwa na vipaumbele vya kitaifa, rasilimali, utekelezaji na upimaji wa matokeo ili yaweze kuleta mabadiliko.”
Wiki ya Ubunifu inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuibua mawazo mapya na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wataalamu, wabunifu na wadau wengine, ili kuhakikisha ubunifu unatumika kama nyenzo ya kutatua changamoto na kuchochea maendeleo kuelekea Tanzania tuitakayo ifikapo mwaka 2050.