Na Albert Kawogo
MWANZO mwa wiki hii Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi, alifanya ziara ya kiserikali nchini na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kufika kwa El Sisi nchini ni muendelezo wa mahusiano mema ya Tanzania na Misri yaliyojengwa tangu miaka ya 70 na viongozi watangulizi wa Mataifa haya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika ziara inayoelezwa ni ya kimkakati zaidi marais hawa wawili walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa kuchunguza uwezekano wa kuanzisha mradi wa pamoja wa kilimo nchini Tanzania, kupanua Bandari ya Dar es Salaam na kufanya utafiti wa kuanzisha njia ya moja kwa moja ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari kati ya Safaga nchini Misri na Dar es Salaam ili kuongeza biashara na kuimarisha uunganisho wa kikanda.
Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Rais El-Sisi alisema viongozi hao walijadili kuanzishwa kwa mradi wa kilimo cha kisasa na uendelezaji wa ardhi nchini Tanzania utakaosaidia kufanikisha usalama wa chakula kwa mataifa yote mawili, kukidhi mahitaji ya ndani ya mazao muhimu ya kimkakati na baadaye kupanuliwa kwa ajili ya mauzo ya nje.
Rais El-Sisi pia alisisitiza utayari wa Misri kushiriki katika upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
“Nimerudia utayari wa Misri kushiriki katika upanuzi na maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam,” alisema, akibainisha umuhimu wa kuunganisha mradi huo katika dira pana ya kuendeleza njia za kikanda za usafirishaji na usambazaji zinazoiunganisha Tanzania na nchi jirani.
Aliongeza kuwa viongozi hao pia walijadili kuanzishwa kwa njia ya usafirishaji wa baharini kati ya Bandari ya Safaga na Dar es Salaam pamoja na kuanzisha ukanda wa usafirishaji wa njia mbalimbali (multimodal corridor) unaounganisha Cairo na Dar es Salaam kupitia miradi kadhaa ya pamoja ya maendeleo.
Rais El-Sisi alisema Misri inalenga kujenga juu ya mafanikio yaliyopatikana kupitia kampuni za Misri katika ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere kwa kushiriki pia katika miradi mingine ya maendeleo nchini Tanzania.
“Nimethibitisha matarajio yetu ya kujenga juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana na kampuni za Misri katika utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere kwa kufungua fursa kwa kampuni zetu za kitaifa kushiriki katika miradi mingine ya maendeleo nchini Tanzania,” alisema.
Misri imetekeleza miradi mikubwa nchini Tanzania, ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji.
Mradi huo wenye thamani ya dola bilioni 2.9 za Marekani ulizinduliwa mwaka 2017 na ujenzi wake kuanza mwaka 2019. Unafadhiliwa kikamilifu na Serikali ya Tanzania na unajengwa na muungano wa kampuni za Misri unaojumuisha Arab Contractors inayomilikiwa na Serikali ya Misri pamoja na Elsewedy Electric.
Bwawa hilo ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya miundombinu barani Afrika ambalo limekamilisha wazo la muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alionyesha nia ya kuanzisha mradi huo miaka ya 70.
Bwawa limesaidia kudhibiti mafuriko pamoja na kupunguza tatizo la upungufu wa umeme nchini Tanzania kwa kuzalisha nishati hiyo kwa zaidi ya watu milioni 60.
Umeme unaozalishwa na mradi huo unasafirishwa kupitia mfumo wa msongo wa kilovolti 400 hadi kituo cha kupokea na kusambaza umeme kabla ya kuunganishwa katika gridi ya taifa, hatua inayotarajiwa kuongeza maradufu uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme.
Rais El-Sisi pia alisema Misri itaongeza msaada wa kiufundi pamoja na programu za mafunzo ili kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania katika sekta mbalimbali.
Viongozi hao pia walishuhudia utiaji saini wa Hati Mbili za Makubaliano (MoU) zinazohusu sekta za uchukuzi, umeme na nishati jadidifu.
Katika mazungumzo hayo, Rais El-Sisi alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa tena kuongoza Tanzania kwa muhula wa pili na kusisitiza dhamira ya Misri ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili katika sekta zote.
Kwa upande wake, Rais Samia alimkaribisha Rais El-Sisi na kuipongeza Misri kwa nafasi yake muhimu barani Afrika na kimataifa, akieleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Misri ni mfano wa mafanikio ya mtangamano wa Afrika unaotarajiwa kufikiwa
Mbali na uhusiano wa pande mbili, viongozi hao walijadili maendeleo ya kikanda, ikiwemo hali ya Mashariki ya Kati, Pembe ya Afrika, Bahari ya Shamu na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa Afrika.
Rais El-Sisi pia alieleza matumaini yake kuwa Tanzania itaendelea kuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha mazungumzo na ushirikiano miongoni mwa nchi za Bonde la Mto Nile.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia aliandaa chakula cha mchana cha heshima kwa ajili ya Rais El-Sisi, ambapo viongozi hao walisisitiza dhamira yao ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara hiyo na kuinua uhusiano wa Tanzania na Misri hadi kiwango cha ushirikiano wa kimkakati.
Ziara ya sasa ya Rais El-Sisi ni ya pili nchini Tanzania. Ziara yake ya kwanza ilifanyika Agosti mwaka 2017, alipokutana na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kupanua ushirikiano wa kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za Wakala Mkuu wa Takwimu wa Misri (CAPMAS), mauzo ya bidhaa za Misri kwenda Tanzania yaliongezeka kwa asilimia 3.2 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, na kufikia Dola Milioni 11.1 za Marekani kutoka Sola Milioni 10.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Hata hivyo, bidhaa zilizoagizwa na Misri kutoka Tanzania zilipungua kwa asilimia 75.8 na kufikia Dola Milioni 1.2 kutoka Dola Milioni 5 mwaka uliotangulia. Kutokana na hali hiyo, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilipungua kwa asilimia 21.6 na kufikia Dola Milioni 12.3 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 ikilinganishwa na Dola Milioni 15.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Bidhaa zilizoongoza kwa mauzo kutoka Misri kwenda Tanzania ni mashine na vifaa vya umeme vyenye thamani ya Dola Milioni 3.1, zikifuatiwa na bidhaa za chumvi na madini ya salfa zenye thamani ya Dola Milioni 1.8, plastiki na bidhaa zake zenye thamani ya Dola Milioni 1.1, sukari na bidhaa za sukari zenye thamani ya karibu Dola 981,000, pamoja na bidhaa za chuma na vyuma zenye thamani ya takribani Dola 796,000.