RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na India umeendelea kuimarika na kuchochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 19, 2026, alipokutana na Makamu wa Rais wa India, C. P. Radhakrishnan, katika Afisi ya Makamu wa Rais wa India (Vice-President’s Enclave), jijini New Delhi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameiomba India kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, afya, teknolojia, Uchumi wa Buluu, uwekezaji na mabadiliko ya kidijitali, huku akialika makampuni na wawekezaji wa India kuwekeza Zanzibar katika sekta za kimkakati.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa India, C. P. Radhakrishnan, amepongeza maendeleo ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi na kusisitiza kuwa India itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, elimu, afya, nishati, huduma za kidijitali na kujenga uwezo wa rasilimali watu.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi na Mkewe, Mama Mariam Mwinyi, walitembelea Eneo la Kumbukumbu la Hayati Mahatma Gandhi (Raj Ghat) jijini New Delhi na kuweka shada la maua kwa heshima ya kiongozi huyo wa harakati za uhuru wa India na mtetezi wa amani.
Ziara ya Rais Dkt. Mwinyi nchini India inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Zanzibar, Tanzania na India, hususan katika sekta za elimu, biashara, uwekezaji, afya, teknolojia na Uchumi wa Buluu, pamoja na kufungua fursa mpya za maendeleo na uwekezaji zenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.