Na Mwandishi Wetu, CHINA
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amewasilisha mafanikio ya Tanzania katika maendeleo na usimamizi wa Akili Unde (AI) wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Juu wa Dunia kuhusu AI uliofanyika jijini Shanghai, China.
Kairuki alisema, Tanzania inaunga mkono juhudi za Kimataifa za kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa AI unaozingatia maadili, usalama na ushirikiano wa Kimataifa.
Alieleza kuwa, AI ni nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo katika sekta za kilimo, afya, elimu, utawala wa kidijitali na uchumi wa kidijitali.
Alibainisha kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inaendeleza mradi wa JAMII AI, mfumo wa lugha ya Kiswahili utakaowanufaisha zaidi ya watu Milioni 200.
Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya kidijitali ikiwemo vituo vinne vya mikongo ya bahari, ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Data za AI na Taasisi ya Teknolojia ya Kidijitali ya Dodoma ili kukuza ubunifu na matumizi salama ya AI.
Akihitimisha, Kairuki alitoa wito kwa mataifa kushirikiana kujenga mfumo wa utawala wa AI unaolinda utu wa binadamu, unaoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na kuhakikisha manufaa ya AI yanawanufaisha watu wote.