WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, aimezitaka Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kuachana na utendaji wa mazoea na kujielekeza katika uongozi unaozingatia matokeo, ubunifu, uwajibikaji na ushirikiano wa karibu na sekta binafsi ili kuharakisha utekelezaji wa DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Prof. Mkumbo alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali yanayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika chini ya kaulimbiu “Kutoka Maono mpaka Matokeo: Kufungamanisha Utendaji wa Mashirika ya Umma na DIRA 2050.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkumbo alisema Tanzania imeweka lengo la kufikia uchumi wa kati wa juu na kukuza Pato la Taifa (GDP) kutoka dola za Marekani bilioni 85 hadi dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 kupitia DIRA 2050.
Alisema mafanikio ya DIRA hiyo hayatategemea ubora wa sera na mipango iliyoandaliwa pekee, bali uwezo wa viongozi wa Taasisi za Umma kutafsiri maono hayo kuwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
“Jukumu mlilonalo ni kubwa. Tunahitaji viongozi wenye maono, uwajibikaji, ubunifu na uadilifu watakaoweza kutafsiri DIRA 2050 kuwa matokeo yanayopimika,” alisema.
Prof. Mkumbo alisema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, ushindani wa kimataifa wa kuvutia uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya masoko ya dunia, hivyo Taasisi za Umma hazina budi kubadilika ili ziwe sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo.
Alisisitiza kuwa Serikali haitapima mafanikio ya taasisi kwa idadi ya vikao vinavyofanyika au taarifa zinazoandaliwa, bali kwa matokeo yanayopatikana kupitia utoaji wa huduma bora, ongezeko la tija, uwekezaji, ajira na mapato ya Serikali.