BANDARI ya Bukoba imepata uso mpya baada ya kukamilika kwa mradi wa ukarabati na upanuzi wenye thamani ya Shilingi bilioni 19.5, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea biashara katika Kanda ya Ziwa Victoria.
Mradi huo uliotekelezwa kuanzia Januari 2023 hadi mwaka 2025 umehusisha ujenzi wa gati jipya la kisasa, ukarabati wa magati mawili ya zamani yaliyokuwa yamechakaa na ujenzi wa kizuizi kipya cha kuzuia upepo mkali (breakwater).
Kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu, maboresho hayo yanalenga kuifanya bandari hiyo kutoa huduma kwa miezi 12 ya mwaka bila kukatizwa na changamoto za mvua na mawimbi makali ya ziwa, ambazo awali zilikua kikwazo kikubwa kwa wamiliki wa meli na wafanyabiashara.
Kukamilika kwa bandari hiyo kunatarajiwa kupunguza gharama na muda wa kusafirisha mizigo kwenda mikoa ya Mwanza, Geita na Kigoma, ambayo inategemea mtandao wa usafiri wa majini.
Zaidi ya soko la ndani, Bandari ya Bukoba inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika biashara ya kikanda, kutokana na ukaribu wake na nchi jirani ya Uganda. Wafanyabiashara wa nchi hizo mbili wanatarajiwa kunufaika na huduma za uhakika za kuhifadhi na kupakua mizigo.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wa majini wanasema mafanikio ya uwekezaji huo hayatapimwa kwa majengo pekee, bali kwa kupungua kwa tozo za bandarini, kasi ya kuhudumia meli na kuongezeka kwa meli zitakazotumia bandari hiyo.
Serikali inatarajiwa kuizindua rasmi bandari hiyo iliyoboreshwa mwishoni mwa mwezi Oktoba 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usafiri wa majini na kuifanya Ziwa Victoria kuwa barabara kuu ya biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.