RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo, tarehe 30 Juni 2026, alipokutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Mhe. Mohammad Javad Hemmatpanah, aliyefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika sekta za elimu, teknolojia, viwanda, kilimo, afya, biashara, mafuta na gesi, huku akiikaribisha Iran kuwekeza Zanzibar, hususan katika uchumi wa buluu na viwanda.
Kwa upande wake, Balozi Hemmatpanah amepongeza uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi kwa mageuzi ya maendeleo Zanzibar na kueleza dhamira ya Serikali ya Iran ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Zanzibar kupitia uwekezaji, kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia katika sekta mbalimbali.