Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema, hakuna Mtanzania anayebaguliwa kwenye sekta ya utalii na kuwataka Watanzania wapuuze maneno yanayotolewa na wasioutakia mema Muungano.
Akizungumza Visiwani Unguja jana, Juni 21, 2026, Mbeto alisema amekuwa Kamishna wa Kamisheni ya Utalii kwa miaka 15, anaijua vizuri sheria ya uwekezaji Tanzania, au Zanzibar kupitia ZIPA, imemtaja wazi Mzawa ni raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sheria ile ikasema, mzawa ni raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kaitazameni sheria ya ajira, inamtafsiri mzawa ni nani, kwa maana hiyo tulichokuwa tunakusudia, unapokuwa na soko kubwa la utalii, watu wanatoka sehemu mbalimbali, watu wanatoka Italy, Comoro, watu wanatoka sehemu nyingine nje ya Tanzania, kwa maana hiyo sheria ile haijambagua Mtanzania hata kidogo,”
Alisema, hivisasa ukienda kwenye maeneo ya kazi, utakuwa watu kutoka Bara na Visiwani wanafanya kazi kwa pamoja na akatolea mfano kwenye makampuni ya ujenzi yanayotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara, wote wanaoendesha mitambo, wanatoka Tanzania Bara na wamesoma Chuo cha Usafirishaji.
“Zanzibar hakuna ubaguzi wa ajira, ajira inatokana na sifa na uwezo wako, ukiangalia kwenye taasisi zetu za ubora, kama tunataka kupima ubora wa jambo, kama kile kipimo hatukipati kwenye maabara zetu tunakwenda Tanzania Bara,”
“Katika eneo hili nawahakikishia hakuna ubaguzi wa aina yoyote na wala hakuna Mtanzania yeyote aliyekwenda hospitali akakosa huduma, au mmeshasikia kuna mtu akatupwa nje akaambiwa hatibiwi? Haya ni maneno yanayosemwa na watu wasioutakia mema Muungano wetu,” alisisitiza Mbeto.
Aidha, Mbeto aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa zozote ambazo zinapatikana kwenye upande mmoja wa Muungano, huku akiweka wazi kwamba, Wazanzibar wananufaika kwa kutumia ardhi ya upande wa pili kwa kuishi na kufanya shughuli zao nyingine, “hili hamlioni? Wanasiasa wenzangu wafikirie kwa kina, tuendelee kudumisha Muungano, tuendelee kudumisha amani na utulivu, sisi sote ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna raia Mzanzibar.”
Alisema, Watanzania wote ni wakaazi na sheria imewekwa wazi kwamba, ukiwa umetoka Tanzania Bara, ukikaa miaka 10 mfululizo unapata kitambulisho cha Mzanzibar. “Ndugu zetu kutoka Tanzania Bara mnakaribishwa, hapa ni kwenu, mna haki ya kutumia fursa zilizopo kama sisi tunavyotumia fursa za upande wa pili.”