Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WANANCHI wameiomba Serikali kupitia kwa Wakala wa Vipimo (WMA) kufanya uhakiki wa vipimo katika bando za Intaneti na muda wa maongezi wanaonunua kupitia kwenye kampuni za simu za mkononi nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye banda la WMA, wanaoshiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kwenye viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma, wananchi hao walisema, bando wanazonunua zimekuwa zikiisha kabla ya muda wake, jambo ambalo ni kinyume na matangazo yanayotolewa na kampuni hizo.
“Unanunua bando ya Shilingi 3,000 au 5,000 kwa wiki, unapiga siku moja au mbili, unaambiwa bando lako limekwisha, ni nani anafanya uhakiki wa hivyo vitu?”
“Sisi tunasema, Serikali kwa namna moja ama nyingine au nyie ambao mnashughulika na suala la vipimo, naombeni mlifanyie kazi,” alisema mmoja wa wananchi hao na kusisitiza, suala hilo linagusa moja kwa moja uchumi wa mwananchi.
Mwananchi mwingine, Yusta Sudi alisema wamekuwa wakinunua vifurushi, lakini havikai kama ambavyo kampuni za simu zinavyowaahidi wanapotaka kujiunga na huduma zao “ombi langu kwa Serikali, kupitia kwa wakala wa vipimo, waliangalie jambo hili,”
Naye, Mwanahamisi Hemedi, mwanafunzi wa Chuo cha Mipango alisema, wanapata changamoto kubwa kwenye upande wa bando za intaneti, ambapo wanajiunga, lakini wanashindwa kuzitumia, hivyo ni vema Serikali ikatupia jicho sekta ya mawasiliano kwa ujumla na kufanya maboresho.
Kwa upande wake Said Ibrahim, Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma alisema, wamepata malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai kwamba, vifurushi vyao vinaisha kabla ya muda, jambo ambalo wameanza kulifanyia kazi.
“Ni jukumu letu kubwa kuhakikisha tunamlinda mlaji na hasa watumiaji wa bando na muda wa maongezi, kwahiyo Serikali kupitia wakala wa vipimo imeshaanza kufanya mchakato wa kufanya majadiliano na mamlaka mbalimbali kwa ajili ya kuhakiki matumizi ya bando na muda wa maongezi,” alisema Ibrahim.
Meneja huyo alisema, mbali na wananchi hao, wabunge wamekuwa wakiuliza kuhusu mkakati wa WMA kuanza kuhakiki muda wa maongezi “napenda kuujulisha umma kwamba, wakala wa vipimo umeanza kufanya mchakato wa kuhakiki bando na muda wa maongezi.”