RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa wananchi kuufanya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria kuwa wa maridhiano, upendo na ustahamilivu, akisisitiza kuwa amani na umoja ni msingi wa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza leo, Juni 15, 2026, katika Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu yaliyofanyika Msikiti wa Jamiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wananchi kuheshimiana, kulinda maadili na kujiepusha na mambo yanayoweza kuleta mgawanyiko.
Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuimarisha amani, maadili na ustawi wa jamii, huku akipongeza mchango wa taasisi hizo katika kuhimiza maadili mema nchini.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na wadau wote kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho hayo, pamoja na viongozi wa dini kutoka Afrika Mashariki walioshiriki katika hafla hiyo.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza Juni 17, 2026 kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria.