WAKAGUZI kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Lakshmikanth Karunanithi na Eduard Captan, wamefanya ukaguzi wa miundombinu ya viwanja vinavyotarajiwa kutumika katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), na kueleza kuridhishwa na hatua ya maboresho yanayoendelea.
Katika ziara hiyo, wakaguzi hao walitembelea Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo walikagua maendeleo ya maboresho ya sehemu ya kuchezea (pitch), maeneo maalumu ya wageni na viongozi mashuhuri (VVIP), pamoja na sehemu zitakazotumika na wanahabari wakati wa mashindano.
Mbali na Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujumbe huo pia ulitembelea viwanja vya mazoezi vya Gymkhana II na Faras, ambavyo vinajiandaliwa kuhudumia timu zitakazoshiriki AFCON 2027.