TIMU ya wataalamu kutoka Tanzania imeshiriki katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 28 wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) uliofanyika jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Heshima wa Mkutano Mkuu wa 28 ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Group 7X (Posta ya Umoja wa Falme za Kiarabu), Badr Al-Olama.
Akihutubia wakati wa ufunguzi, Al-Olama alisema kuwa mkutano huu ni fursa ya kuweka msingi wa utoaji wa huduma za posta katika mazingira ya ushindani wa kiteknolojia na mabadiliko ya mahitaji ya wateja.
“Sekta ya Posta lazima iendelee kuwa imara na mhimili wa huduma kwa wananchi katika karne ya 21,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa UPU, Masahiko Metoki, alisema kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuhakikisha kila mshiriki wa mtandao wa Posta anachangia kukuza biashara na huduma duniani.
“Ni muhimu kushirikiana ili mtandao wa posta uendelee kuwa thabiti na chachu ya maendeleo ya biashara na huduma,” aliongeza.
Mkutano Mkuu wa UPU ni chombo cha juu cha maamuzi kinachowapa wanachama nafasi ya kujadili na kupitisha mapendekezo yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa za posta, mifumo ya malipo, ubora wa huduma, biashara mtandao, na kuimarisha uthabiti wa mtandao wa Posta hususan kwa nchi zinazoendelea.
Mkutano huu unawakutanisha watunga sera, wadhibiti, taasisi za Posta na watoa huduma binafsi duniani kote.
Umeanza rasmi Septemba 8, 2025 na unatarajiwa kuhitimishwa Septemba 19, 2025 jijini Dubai.