RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehimiza kuimarishwa kwa diplomasia ya uchumi baina ya Zanzibar na Japan.
Akizungumza Ikulu Zanzibar leo Septemba 9, 2025 na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Anderson Gukwi Mutatembwa, Dkt. Mwinyi alisema Japan ina wawekezaji wengi ambao Zanzibar inawakaribisha kuwekeza hususan katika uchumi wa buluu, biashara ya mwani, utalii, michezo, mafuta na gesi.
Aidha, alibainisha kuwa Zanzibar inalenga kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za baharini na hivyo ni muhimu kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Japan.
Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alimhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuweka mkazo katika kusimamia ushirikiano wa kiuchumi na miradi ya maendeleo kati ya Japan na Tanzania, ikiwemo Zanzibar.