Mradi wa TACTIC waboresha usafiri na usafirishaji Sumbawanga

0

MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa baada ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Sumbawanga, Nassir Kilusha ambapo amesema kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 20.361 zimepokelewa kupitia mradi wa TACTIC kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi kwa wasimamizi wa mradi, ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilomita 13.3 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa mitaro pamoja na uwekaji wa taa za barabarani ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia zaidi ya 80.

“Kabla ya mradi barabara zilikuwa na vumbi, mashimo, matope na maji kujaa katika makazi ya watu na kusababisha kero kwa wananchi lakini sasa maji hayatuami,biashara zinafanyika hadi usiku kwasababu ya taa, uwekezaji umeongezeka, usalama umeongezeka, thamani ya viwanja na nyumba imepanda pia shughuli za usafiri na usafirishaji zimeongezeka”, alisema.

Kilusha ameongeza kuwa sasa wanaendelea na ujenzi wa Soko kuu la mazao ya nafaka eneo la Kanondo ambalo litaongeza thamani ya mazao likijumuisha maegesho ya magari, eneo la mawakala, maghala ya kuhifadhia mazao na eneo la kuuzia chakula (baba lishe na mama lishe) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7.4 ujenzi unaotarajiwa kukamilika Desemba 2025.

Kuhusu mapato ya Halmashauri, Kilusha ameeleza kuwa mwaka wa fedha uliopita walikuwa wanakusanya Shilingi Bil. 3.4 lakini mwaka huu wa fedha wanatarajia kukusanya Shilingi Bil. 3.9 kutakuwa na ongezeko la Shilingi Milioni 500 ambapo amewataka wananchi kuilinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here