Wananchi Korogwe wahamasishwa kujiunga na bima ya afya

0

NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, ameendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya ili kuondoa usumbufu wa gharama za matibabu.

Prof. Nagu amesema hayo wilayani Korogwe mkoa wa Tanga wakati akihitimisha ziara ya usimamizi shirikishi ya kutembelea vituo vya kutolea huduma za Afya na kuzungumza na watumishi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.

“Katika kuhakikisha huduma hizi za Afya zinaendelea ni muhimu wananchi waweze kugharamia na njia bora ya kugharamia huduma za afya ni kwa kuwa na bima tunatoa rai kwa wananchi wote kila mmoja na kila familia kujiunga na bima ya Afya ili wakati wa kupata changamoto fedha zisije kuwa kikwazo.” alisema.

Amewaomba watumishi kuwa mabalozi wa kuwahamasisha wananchi wanajiunga na Bima ya Afya kuanzia nyumbani hadi kwenye maeneo wanayotolea huduma.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Mji, Mwashabani Mrope, amepokea maelekezo hayo na kusema Halmashauri hiyo itaendelea kutekeleza maagizo ya serikali kwa kuboresha huduma za Afya.

Naye Juma Mhina, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwamsisi, ameishukuru serikali kwa ujenzi wa kituo cha Afya, kwani kinawasaidia kupata huduma kwa urahisi na haraka tofauti na mwanzo walipokuwa na jengo moja lililokuwa na ufanisi mdogo wa kutolea huduma.

Prof. Nagu yupo mkoani Tanga kwaajili ya ziara ya usimamizi shirikishi akiwa ambatana na wataalamu wa Afya kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI lengo likiwa ni kuendelea kuhamasisha ubora wa huduma za Afya kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here