Rais Mwinyi: Dira ya 2050 ni nyenzo ya maendeleo kwa Taifa

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iliyohitimishwa na kutoa rai kwa Watanzania kuipokea kwa dhati Dira mpya ya 2050 kama nyenzo ya maendeleo ya Taifa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 17, 2025, alipotoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.
 

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na wananchi kwa ujumla, wanajivunia hatua kubwa zilizofikiwa kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, hatua ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni mwanzo mpya wa maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo na kwamba mchakato wake wa uandaaji ulikuwa wa wazi, shirikishi na wa kitaalamu, uliowapa fursa Watanzania kutoka makundi mbalimbali kushiriki na kutoa maoni yao.

 
Rais Dkt. Mwinyi amehitimisha salamu zake kwa kutoa wito kwa Watanzania wote, kuisoma kwa kina Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuelewa vema mwelekeo wa Taifa, na kila mmoja aweze kutambua na kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Katika hotuba yake ya uzinduzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amezitaka Wizara na Taasisi zote za Serikali kupitia upya sera zao ili ziendane na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga maendeleo jumuishi ya Taifa.

Aidha, ameziagiza sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa malengo ya dira hiyo, akisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kufikiwa bila mshikamano wa sekta zote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here