Zoezi la maboresho ya daftari la wapiga kura kuanza Mei 16 Kibaha DC

0

WADAU wa vyama vya siasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wamekutana kwa ajili ya kujadili maandalizi ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Vyama vilivyoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na Chama cha CCJ.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti Edward Masona ametoa wito kwa vyama hivyo kwenda kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, hususan wale ambao hawakubahatika kuboresha taarifa zao awali.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wananchi ambao taarifa zao zilikuwa na makosa au waliohama makazi kujitokeza katika vituo husika kwa ajili ya kufanya marekebisho.

Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Grace Haule, amewakumbusha wadau wa siasa kuzingatia sheria na kanuni za Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa amani na bila migogoro isiyo ya lazima.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Gabriel Mziwanda, Katibu wa chama cha CCJ, na Mohamedi Ngozi, Katibu wa chama cha NCCR-Mageuzi, wameahidi kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kufanya maboresho ya taarifa zao.

Zoezi la maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuanza rasmi Mei 16, 2025, na litadumu kwa muda wa siku saba katika vituo 19 vilivyopangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here