Zijue sababu za Hifadhi ya Kitulo kuitwa bustani ya Mungu

0

Na Cecilia Mwashihava

HIFADHI ya Kitulo inapatikana Nyanda za juu Kusini mwa Tanzania katika Jiji la Mbeya na Mkoa wa Njombe. Hifadhi hii ipo kati ya kilele cha Milima ya Kipengere na Poroto, pia linajumuisha Safu za Milima ya Livingstone.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ina ukubwa wa Kilomita za mraba zipatazo 412.9. Hifadhi hii ni ya kwanza kabisa ya Kitaifa katika Afrika ya Kitropiki kuanzishwa kwa lengo mahususi la kulinda na utunzaji wa mimea yake asilia ambayo sehemu kubwa ni maua.

Hapo awali, Hifadhi ya Kitulo ilijulikana kama ‘Elton Plateau’ baada ya kugundulika na Fredrick Elton baada ya kupita eneo hili mnamo mwaka 1870. Baadaye, mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hili na kulitumia kwa matumizi ya kilimo cha ngano na ufugaji wa kondoo, baadaye lilikuja kugeuzwa kuwa shamba la ng’ombe ambalo bado lipo mpaka sasa.

Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa eneo hili la Hifadhi ya Kitulo, watu mbalimbali na wadau wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kama hifadhi ya Taifa ili kulinda aina mbalimbali za maua na mimea adimu inayopatikana pekee katika eneo hili.

Hifadhi ya Kitulo ilianzishwa mwaka 2002 na Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa na kutangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa na Serikali mwaka 2005 na kuanzia hapo ikawa Hifadhi ya Taifa ya Kumi na nne (14) nchini Tanzania. Hifadhi hii inasimamiwa na kuratibiwa na Hifadhi za Taifa za Tanzania (TANAPA).

Watu wengi hupendelea kuiita Hifadhi hii ‘Bustani ya Mungu’. Hii ni kutokana na uzuri wa hifadhi hii uliopambwa na aina mbalimbali za maua mazuri yakuvutia yenye rangi nzuri na harufu za kipekee na mengi kupatikana hifadhi ya Kitulo pekee Duniani kote. Wataalamu wa mimea huiita ‘Serengeti ya Maua’ kutokana na utajiri wa aina nyingi za maua yanayopatikana ndani ya hifadhi na kuifanya kuwa moja ya sehemu ya maonesho ya maua mazuri Duniani.

Hifadhi ya Kitulo ina spishi tofauti za maua zipatazo 350 ambapo aina 40 za maua haya hazipatikani popote duniani na aina 45 za okidi za ardhini ambazo huibuka na maua ya viwango tofauti wakati wa mvua kuu mwishoni mwa mwezi Novemba mpaka Aprili kila mwaka.

Upekee wa hifadhi ya Kitulo ni pamoja na kuwepo kwa ndege aina ya tandawili machaka ‘Denhams bustard’ wenye uwezo wa kuruka kutoka Bara moja hadi jingine. Hifadhi ya Kitulo ndiyo eneo pekee ndege hawa hutaga mayai na kuzaliana kwa wingi kabla ya kwenda katika mabara mengine.

Katika misimu fulani ndege hawa huruka na kufika katika hifadhi ya Kitulo kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi hii kuwa ni mahali pekee duniani yenye hali ya hewa rafiki kwa ndege hawa kuzaliana.

Hivyo, baada ya kutaga mayai, mayai huanguliwa na vifaranga hao kukua ndipo huruka na kwenda mabara mengine. Tafiti zinaonesha, kuna ndege aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama wakiwa katika hifadhi ya Kitulo na baadae kuonekana katika bara la Australia wakiwa na alama zile zile walizowekewa katika hifadhi ya Kitulo.

Hifadhi ya Kitulo hupatikana pia ndege aina mbalimbali tofauti na tandawili machaka ambao ni ‘Abdims stock’, ‘blue swallow’, mpasua mbegu mweusi (kipengere seed eater) na wengineo ambao wametoka sehemu mbalimbali kama Afrika Kusini, Afrika Kaskazini, Australia na Ulaya na hutumia hifadhi ya Kitulo kama eneo lao la makazi katika misimu tofauti tofauti ya mwaka.

Pia, hifadhi ya Taifa ya Kitulo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo jamii mpya ya nyani (Lophocebus kipunji) ambao waligundiliwa mwaka 2003 katika hifadhi ya Kitulo, vipepeo wa aina mbalimbali hupatikana nao ambao husaidia kuchavusha maua ya hifadhi hii na kuipamba Kitulo kwa uzuri wakiwa wanaruka ruka, bila kuacha vinyonga, mijusi na vyura ambao huongeza utajiri wa kibailojia katika hifadhi ya Kitulo.

Licha ya kuwa na maua aina mbalimbali hifadhi ya Kitulo inao uwanda wa tambarare, mabonde, vilima na maporomoko ya maji pamoja na mabwawa (muhimu kwa mto Ruaha) ambavyo ni vivutio vikubwa vya watalii wengi wanaofika hifadhi ya Kitulo hasa kwa utalii wa picha na mazingira ‘adventure tourism’.

Ukifika katika hifadhi ya taifa ya Kitulo unaweza kupata fursa ya kutembelea Milima ya Livingstone ambao upo karibu na Ziwa Nyasa, kupanda farasi na michezo ya gofu. Hifadhini utafurahia upepo mwanana kutoka mwambao wa Ziwa Zambwe ukisindikizwa na nyimbo nzuri za ndege warukao hifadhini hapo.

Eneo la Kitulo linafikika kwa urahisi kabisa ambalo Kilomita 110 tu kutoka eneo la wilaya ya Mbeya Mjini. Muda mzuri wa kutembelea hifadhi ya Kitulo na kuona utajri wa mandhari nzuri ya maua ni mwezi wa kumi na mbili ‘Disemba’ mpaka mwezi wa nne ‘Aprili,’ ambapo okidi nyingi za maua huchanua na kuwa na maua mazuri yanayovutia.

Kuanzia mwezi wa tisa hadi wa kumi na moja ni muda mzuri wa kupanda mlima, huku mwezi wa sita hadi wa nane ni miezi ya baridi kali. Karibu sana hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa utalii, ujionee bustani hii nzuri iliyopambwa na maua mbalimbali. Unasubiri nini kujionea bustani ya Mungu, unasubiri nini kuona maajabu ya Dunia?

Mwandishi wa Makala hii ni Mhifadhi wa wanyamapori, anapatikana kwa barua pepe;-mwashihavacecilia@gmail.com au 0747 268 217.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here