Zanzibar ni nchi ya makabila tofauti, ACT Wazalendo waache ubaguzi – Mbeto

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

VIONGOZI wa ACT Wazalendo wametakiwa kuacha kubagua watu kutokana na asili zao, kwani Zanzibar ni Kisiwa cha watu mchanganyiko (Cosmopolitans), wenye asili tofauti.

Akizungumza Mjini Unguja, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Mbeto Khamis Mbeto, alisema si sahihi ACT Wazalendo kutoa kauli za kibaguzi kwa watu wa kabila la Wamasai.

Alisema, kinachotakiwa ni kuangalia sifa zinazotakiwa mtu kuwa nazo kabla ya kupata kitambulisho cha Ukaazi na kile cha kupigia kura na sio kumbagua kwa kabila lake.

Mbeto alisema, Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar namba 4 ya mwaka 2018 Ibara ya 15 kifungu cha 6 na 7 inasema moja ya sifa ya kuandikishwa uwe na kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi.

Alibainisha kuwa, Sheria ya Utambuzi, Vizazi na Vifo namba 3 ya 2018 inasema kila Mzanzibari, aliyezaliwa Zanzibar na kufikisha miaka 18 ana haki ya kupata Kitambulisho cha Mnzanzibari Mkazi.

Pia, inaendelea kusema Sheria hiyo kuwa, Mtanzania yeyote aliyeishi Zanzibar miaka 10 mfululizo ana haki ya kupata kitambulisho hicho cha Ukaazi.

Mbeto alisema, watu wa kabila la Wamasai waliingia kwa wingi Zanzibar miaka ya tisini wakati Serikali ya Mapinduzi (SMZ), ilipofungua milango katika sekta ya utalii.

Alisema, mwenye kumbukumbu nzuri, watu wa kabila hilo, wengi walikuja kufanyakazi za ulinzi kwenye hoteli za mwanzo visiwani humo.

“Kuna Masai walikuja miaka ya tisini na baadhi yao hawajaondoka hadi leo walikuwa wakifanyakazi za ulinzi Veta Club na wengine, hoteli ya Mawimbini,” alisema.

Mbeto alibainisha kuwa, Zanzibar ni nchi ya raia wenye asili za makabila na Mataifa tofauti akitolea mfano, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu ambaye ana asili ya India.

“Wapo wengi kina Mazruhi haya majina asili yao Oman, wakapita Mombasa na kuingia Pemba,” alisema Mbeto.

“Kinachofanywa na chama hicho kwa sasa ni ubaguzi ambao ulizikwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na Rais wa Kwanza, Abeid Amani Karume.”

“Ili kuondoa dhana ya ubaguzi na jamii zingine kujiona bora zaidi ya zingine, Rais huyo wa kwanza, akataka watu wa asili tofauti kuchumbiana na kuoana.”

Mbeto alisema, mtandao wa biashara ya utumwa ambayo ilipigwa marufuku mwaka 1873, ulileta watu kutoka Nyasa, DR Congo, Ujiji Kigoma, Tabora, Shinyanga na kwingineko hadi Zanzibar.

Alibainisha pia, kuna Wangazija, Waajemi, watu kutoka Bara Hindi, Oman na Mataifa mengine mengi ambao vizazi vyao vimebaki hadi hivi sasa.

“Leo wanasema mara ooh mbona waMasai wanapewa vitambulisho vya kupigia kura wenye sifa wanaachwa,” alisema Mbeto na kubainisha kuwa huo ni ubaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here