π Lengo ni kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi
WIZARA ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeeleza kuwa zaidi ya miti 94,000 imepandwa katika Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma (Ring Road) ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Mazingira na Jamii kutoka TANROADS, Zafarani Madayi mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipotembelea na kukagua banda la Wizara ya Ujenzi na TANROADS katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yaliyofanyika Juni 5, 2026, katika Viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Madai amesema kuwa Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo Mradi wa Kukijanisha Jiji la Dodoma (Green Spine Project – GSP), unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Amefafanua kuwa kupitia mradi huo, ukanda wa kijani (greenbelt) umeanzishwa kuzunguka Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma na Zaidi ya Miti 94,000 imepandwa katika barabara hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amesema hadi kufikia mwezi Juni 2026, miti zaidi ya 94,000 imekwishapandwa, huku ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ukiendelea.
Miundombinu hiyo inahusisha usimikaji wa matanki ya maji na uchimbaji wa visima 11 vitakavyowezesha matumizi ya mfumo wa umwagiliaji wa matone kwa ajili ya kuhakikisha miti hiyo inastawi.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 kimewakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kutoka mashirika, taasisi, wizara na wananchi kwa ujumla, chini ya kaulimbiu isemayo: βDira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.β