Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesifu uwezo, upeo,maarifa na ujasiri ulioonyeshwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa heshima Taifa wakati akijibu maswali katika ziara ya kiserikali nchini Urusi.
Kimeyataja majibu ya Rais Dkt. Samia mbele ya dunia, ni kudhihirisha kiwango cha uelewa wake katika mawanda ya diplomasia na utetezi wa maslahi ya Taifa.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipomzungumzia Rais Dkt. Samia alipofafanua kutokuwepo kwa vikwazo kwa nchi yake.
Akijibu swali aliloliita la mtego, Mbeto alisema, Rais alieleza kinagaubaga nchi yake haijawekewa vikwazo na Taifa lolote duniani na kwamba litabaki kuwa mshirika na Mataifa yote.
Alisema, Rais akijibu kwa utulivu, busara na hekima baada ya kuitaja Tanzania haiko chini ya vikwazo na kwamba imekuwa ikihimiza ushirikiano na Mataifa yote inagawaje haifungamani na Siasa za Taifa lolote.
“Tunampa mkono wa kulia wa hongera Rais Dkt. Samia kwa upeo, maarifa kwa kuonesha kusimamia vema kanuni na misingi ya diplomasia. Amelipa heshima Taifa lake kwa usawa na manufaa ya pamoja.
Aidha, Mbeto alisema aina ya majibu yake, ndio msimamo wa Taifa lolote linalojiamini, linalojitambua na linalotanguliza mbele maslahi ya nchi na watu wake.
“Majibu baada ya swali aliloulizwa, yakapokelewa kwa kushindo cha makofi ya furaha kutoka kwa mwenyeji wake Rais Vladimir Putin na Washiriki wa kongamano la kimataifa la uwekezaji,” alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, Rais Dkt. Samia ameonesha kiwango cha busara, utulivu na umahiri wa kidiplomasia, hivyo amedhihirisha kuwa na ufahamu na uliopevuka kiutawala.
“Nchi yetu itabaki na msimamo wa kuongeza marafiki na Washrika waaminifu. Tanzania haitafuti maadui wala kuchagua kambi za migogoro ya dunia. Itajenga dhima na kudumisha Urafiki, Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano,” alisema Mbeto.
Hata hivyo, Mwenezi huyo alisema milango ya Ushirikiano na udugu wa miaka mingi baina ya Tanzania na Urusi, itaendelea kuwa wazi na kutanua wigo wa shughuli za Kiuchumi, Elimu, Historia na Uwekezaji.