Wizara ya elimu Z’bar yashauriwa kuwafundisha wanafunzi uogeleaji

0

NAIBU Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, ameishauri Wizara ya Elimu kuanzisha mtaala maalum wa kuwafundisha wanafunzi uogeleaji na mbinu za kuokoa maisha katika skuli mbalimbali nchini, ili kuwawezesha kukabiliana na maafa yanapotokea.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kuzama Duniani yaliyofanyika katika Fukwe za Forodhani, Hafidh amesema kuwa hatua hiyo itasaidia wanafunzi kujikinga dhidi ya hatari za majanga ya maji, hasa katika maeneo yaliyo karibu na bahari na mabwawa.

Alisema, asilimia kubwa ya vifo vinavyotokana na maafa ya kuzama hutokana na ukosefu wa uelewa wa uogeleaji na mbinu za kujinusuru, hali inayotishia usalama wa jamii.

Amevitaka pia vikosi vinavyohusika na masuala ya uokozi kuendelea kutoa elimu na mafunzo ya uogeleaji kwa umma ili kuimarisha ulinzi wa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib, alisema Kamisheni hiyo imejikita katika kutoa elimu kuhusu maafa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wakulima wa mwani, na kuimarisha uwezo wa vikosi vya uokozi kwa kuwapatia vifaa na rasilimali watu.

Amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa walinzi wa fukwe na mabwawa ili kurahisisha shughuli za uokozi na kuendeleza ushirikiano wa pamoja, akibainisha kuwa suala la kuzama ni tatizo mtambuka linalohitaji juhudi za pamoja.

Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Uokozi Zanzibar, Lukman Said Issa, ametoa wito kwa jamii kujitokeza katika vyuo kujifunza uogeleaji, akisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa Zanzibar imezungukwa na maji na wananchi wanapaswa kuwa na uwezo wa kujinusuru.

Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Ali Omar, alisema kuwa maafa ya kuzama hayaepukiki kwa asilimia 100, lakini jamii inapaswa kuchukua hatua za tahadhari na kujifunza namna ya kujilinda na kuyakabili.

Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, yaliambatana na mashindano ya kuogelea kwa umbali wa kilomita 1, 5, 25 na 50.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here