Wawekezaji kutoka Saudi Arabia wavutiwa na fursa za Utalii Tanzania

0

WAWEKEZAJI kutoka Saudi Arabia wametembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya SabaSaba, wakijionea fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya utalii na maliasili hapa nchini.

Kiongozi wa msafara huo, Abdulahim Ahmed, amesema wameridhishwa na juhudi za Tanzania katika kuendeleza shughuli za utalii na uhifadhi, akibainisha kuwa kuna nafasi kubwa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika kukuza sekta hiyo.

“Tumefurahishwa na namna Tanzania inavyosimamia vivutio vyake na tunatarajia kushirikiana katika kuviboresha na kuhamasisha wawekezaji kutoka Saudi Arabia kuja kuwekeza hapa,” alisema Ahmed.

Wakiwa katika banda la wizara, wageni hao walipata maelezo kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta za wanyamapori, utalii na malikale, ikiwemo ujenzi wa huduma muhimu kwenye maeneo ya vivutio.

Pia, msafara huo ulitembelea idara mbalimbali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo walijionea shughuli za ufugaji nyuki na bidhaa zinazozalishwa.

Aidha, wawekezaji hao walipata maelezo kuhusu upatikanaji wa mbegu na miche bora, uwekezaji katika mashamba ya miti, biashara ya mazao ya misitu, na matumizi ya teknolojia kudhibiti majanga ya moto misituni.

Maonesho ya SabaSaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kujadili fursa za uwekezaji na ushirikiano, hasa kwenye sekta ya utalii na uhifadhi wa mazingira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here