Watumishi wa afya wenye lugha chafu waonywa

0

Na Angela Msimbira, TARIME

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Mahera amekemea tabia ya baadhi ya watoa huduma za afya kutumia lugha chafu kwa wagonjwa.

Ameyasema hayo kwenye kikao kazi na Timu za Usimamizi wa Huduma za afya za Mkoa na Halmashauri kwa lengo la kujadili hali ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara.

Alisema, kumekuwapo na taarifa za baaadhi ya watoa huduma za afya katika hospitali ya mji wa Tarime kutumia lugha chafu kwa wagonjwa na kusisitiza kuwa tabia kama hizo hazivumiliki.

“Nimepata taarifa kuwa Hospitali ya Mji wa Tarime inachangamoto kubwa sana ikiwemo matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa na kutotoa huduma bora kwa wananchi hili jambo ni halikubaliki na ni kinyume na utaratibu wa sheria za kitabibu,” alisisitiza Dkt. Mahera.

Alisema, timu za usimamizi huduma za afya kuhakikisha wanasimamia na kuhakikisha wanabadilisha tabia za watumishi wa aina hiyo, kwani hawapo juu ya sheria, bali wameajiriwa na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia, amewataka wahakikishe watumishi wa sekta ya afya wanafanyakazi kwa bidii, weledi na uzalendo na kuwa changamoto wanazokabiliana nao wakati wa kutimiza majukumu yao zisiwe fimbo ya kuwanyanyasa wagonjwa wanapohitaji huduma za afya.

Alisema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu, vifaa na vifaa tiba ni wajibu wa kila mtumishi wa afya kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuwaokoa maisha ya watu.

Aidha, amewataka kuboresha hali ya utoaji wa huduma na kuacha tabia kuleana na kutaka kuwafichua wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo ili sheria ichukue mkondo wake na watu kama hao hawahitajiki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here