Wadau watakiwa kutumia huduma za vyuo vya mafunzo ya Amali

0

Na Subira Ally

TAASISI za Serikali na binafsi zimetakiwa kutumia huduma zinazotolewa na vyuo vya mafunzo ya Amali ili kupata huduma bora.

Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Abdulghulam Hussein, alisema hayo huko Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati akifungua kituo Cha Mradi wa mafunzo ya walimu wa mafunzo ya Amali.

Alisema, vyuo vya Amali vimekuwa vikitoa huduma zinazokwenda na mahitaji ya jamii ikiwemo utengenezaji magari, na mapishi ambayo ni muhimu kwa mahitaji ya umma.

Alisema, vyuo vyetu vinaboreshwa ili kutoa huduma zinazoendana na mahitaji , hivyo ni vyema kwa vijana kutumia vyuo hivyo ili kupata ujuzi ulio Bora.

Aidha, aliwasisitiza walimu na vijana kutumia kituo hicho kujiendeleza, kwani kuna kozi mpya zinaendelea kutolewa ikiwemo upishi ambao unahitajika zaidi katika hoteli za kitalii na sehemu nyengine za huduma.

Alisema, dhamira ya Serikali ni kuongezwa vituo vya Amali na kuboresha mazingira, hivyo kufunguliwa kwa kituo hicho kitawawezesha vijana kupata sehemu ya kupata ujuzi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Bakari Ali Silima, alisema matumizi ya Sayansi na Teknolojia ni jambo la lazima kutokana na mahitaji ya ujuzi wa kiufundi katika kujipatia kipato, na muendelezo wa ujuzi na mafunzo ya vitendo yanahitajika katika soko la ajira kwa kiasi kikubwa.

Alisema, njia moja wapo ya kupata wataalamu nchini ni kuwapa walimu mafunzo ya ufundi na nadharia kulingana na mabadiliko ya teknolojia yanayojitokeza.

Alisema, Serikali ina matumaini kwa kupitia vituo vya mafunzo ya Amali hata mafunzo yanayohusu uchumi buluu yatapewa kipaumbele ili kufikia kule Serikali inakotarajia na kuweza kufika kimaendeleo na wananchi wetu ni sekta inayochangia Pato la wananchi na Serikali kwa asilimia kubwa.

Aidha, alibainisha Serikali ya Mapinduzi inaishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuisaidia Zanzibar ili kuona dhamira ya kielimu inafikiwa lengo lililokusudiwa.

Kwa upande wake Meneja mradi wa mafunzo ya Amali baina ya Zanzibar na Ujerumani Hans Dietter Allgaier, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wao wa kuridhia ujenzi wa kituo hicho na kusema wataendelea kutoa ushirikiano na kuisaidia Zanzibar katika ujenzi wa vituo vya Amali.

Nae Mkuu wa kitengo cha upishi Salum Abdalla Haji, alisema wanahitaji kuongezwa vifaa vya mapishi kulingana na mahitaji ya wanafunzi Ili kutoa huduma nzuri kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mkuu wa vifaa vya ufundi Kalhamis Khamis Mohammed alisema, wanakabiliwa na upungufu wa vifaa vya ufundishaji Ulingana na mahitaji ya wanafunzi.

Awali, wakizungumza na mwandishi wa habari mwanafunzi wa chuoni hapo Fatma Fundi Juma na Hamad Mohamed Ngwali walisema, kufunguliwa kituo Cha walimu watapata nafasi nzuri ya kujifunza na kuongezwa maarifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here