Wabunge wa Zambia wajifunza uendeshaji Serikali za Mitaa

0

Na OR-TAMISEMI, Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Zainab Katimba amewapokea wageni kutoka Bunge la Taifa la Zambia ambao wamekuja kutembelea na kujifunza jinsi Mfumo wa Serikali za Mitaa unavyotekelezwa Tanzania Bara.

Akiongea na wageni hao ambao ni Wabunge wa Taifa la Zambia katika ukumbi wa Sokoine TAMISEMI Jijini Dodoma kwa niaba ya Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katimba alisema Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndiyo ina mamlaka mapana na muhimu.

Akitaja Mamlaka hayo alisema, ni Uratibu na Usimamizi wa shughuli za Serikali ngazi ya Mikoa na Serikali za Mitaa, kujengea uwezo wa Serikali za Mitaa, uendelezaji na utekelezaji wa Sera, upangaji na ufuatilaji wa fedha za Serikali za Mitaa.

Mengine ni usimamizi na utoaji wa huduma hasa elimu, afya, na miundombinu, kukuza ugatuaji wa madaraka na utawala bora pamoja na kuwezesha mahusiano baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na utatuzi wa migogoro katika ngazi ya Halmashauri na ngazi ya msingi pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Majukumu haya ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo jumuishi, uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wananchi, na utawala shirikishi – maadili tunayoamini yanashirikishwa katika nchi zetu zote mbili,” alisisitiza Katimba.

Akiongea kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wenzake, Twaambo Mutinta, Mkuu wa Msafara na Mwenyekiti wa Kamati ya Serikali za Mitaa, Makazi na Masuala ya Machifu (Chiefs’ Affairs) alishukuru kwa mapokezi mazuri yaliyofanywa na ofisi ya Rais – TAMISEMI na kusema nchini Zambia Mfumo wa Ugatuaji wa Madaraka ulianza mwaka 2016.

Alisema, kupitia ziara hiyo, watakuwa na wakati mzuri wa kujifunza hapa Tanzania na kubadilishana ujuzi, kwani umuhimu mkubwa unaonekana katika kupeleka rasilimali na maamuzi karibu na wananchi .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here