WAANGALIZI wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria za nchi na kuepuka kuingilia au kushiriki katika vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri au kuingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 wakati wanapotekeleza majukumu yao ya uangalizi.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 17, 2025 na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, wakati akifungua kikao cha siku moja na Waangalizi hao kwa lengo la kuwapa maelekezo, taarifa muhimu na miongozo kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao ya uangalizi wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
Katika hotuba yake, Jaji Asina amewakumbusha waangalizi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uhuru, na kutokuwa na upendeleo, huku wakizingatia sheria za nchi na Mwongozo wa Waangalizi wa Uchaguzi wa mwaka 2025.
“Waangalizi wanapaswa kuepuka kuingilia shughuli za uchaguzi, kutoonyesha dhihaka kwa watendaji wa uchaguzi, au kutoa maelekezo kwa maafisa wa Tume kuhusu namna ya kufanya kazi zao,” amesisitiza Jaji Asina.
Jaji Asina ameongeza kuwa endapo kuna malalamiko au dosari yoyote inayojitokeza, waangalizi hao hawana budi kuwasilisha malalamiko hayo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa njia ya Tume.
Katika kikao hicho, mada tatu kuu ziliwasilishwa kwa waangalizi wa uchaguzi ambapo mada ya Maandalizi ya Uchaguzi iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi mada ya ma Masuala ya Usalama iliwasilishwa na mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania, na mada kuhusu Masuala ya Afya iliwasilishwa na mwakilishi kutoka Wizara ya Afya.