MWENYEKITI wa Bodi ya Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Ame Khamis, amewataka waandishi wa habari wanaoripoti taarifa za uchaguzi kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuepusha migogoro na maafa katika taifa na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika Ukumbi wa Shekhe Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Khamis alisema vyombo vya habari ni taasisi muhimu katika nchi yenye mfumo wa kidemokrasia, hivyo vina wajibu wa kutoa habari sahihi, zenye kujenga na siyo kuchonganisha wananchi.
Alionya kuwa vyombo vya habari vinapokuwa vikitumiwa vibaya kwa maslahi ya watu binafsi, vinaweza kusababisha maafa makubwa kama ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya nchi.
โTunachohitaji ni kuona uchaguzi wa Zanzibar unafanyika kwa amani. Ni muhimu kuepuka habari za uchochezi na uvunjifu wa amani,โ alisema Khamis.
Alisisitiza kuwa, waandishi wanapaswa kufuata maadili ya taaluma pamoja na kanuni za Tume ya Utangazaji na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ili kuepuka matatizo binafsi yanayoweza kujitokeza kutokana na kuripoti kwa pupa au kutozingatia ukweli.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Hiji Dad Shajak, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Zanzibar, walisema kuwa amani wakati wa uchaguzi ni jambo la msingi, hivyo waandishi wanapaswa kuwa makini katika vipindi na taarifa zao kwa kuzingatia miiko ya uandishi.
Naye Mwanasheria wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Khadija Mabrouk Hassan, akiwasilisha mada kuhusu kanuni za huduma za utangazaji wakati wa uchaguzi, aliwataka watayarishaji wa vipindi na vituo vya habari kuwasilisha mpango kazi wao Tume ya Utangazaji Zanzibar kama sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria.
Aidha, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alionya kuwa kipindi cha kampeni ni nyeti na huwa na changamoto za mvutano na upotoshaji wa kisiasa, hivyo waandishi wanapaswa kuepuka upendeleo, taarifa za uongo na kutumiwa kwa maslahi binafsi ya wanasiasa.
Alisisitiza kuwa jambo la kwanza katika kazi za uandishi ni kuangalia mustakabali wa taifa na kulinda maslahi ya wananchi.