Vyuo vikuu nchini vyalipa kipaumbele somo la maadili

0

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya Vyuo Vikuu nchini vimeanza kufundisha somo la maadili ikiwa ni moja ya jitihada za kujenga jamii yenye maadili kuanzia kwenye ngazi za malezi.

Hayo yamesemwa na Fabian Pokela, Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya viongozi, wakati akiwasilisha mada kwenye kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mei 30, 2025.

Poleka alisema, katika kutimiza majukumu yao ya kuhakikisha wanasimamia maadili nchini, wamebuni njia mbalimbali ikiwemo kuatoa elimu kwa ngazi zote, ambapo hivisasa baada ya somo la maadili kuingizwa kwenye mtaala wa shule za Msingi, wanaendelea kufanya mazungumzo na Vyuo Vikuu ili wafundishe somo hilo kwa ngazi hiyo ya juu.

“Mashuleni tumeanzisha Klabu za maadili, hizo zipo za kutosha, lakini kumeanzishwa mtaala wa maadili, kwenye somo la Uraia, ndani kuna somo la maadili, ni jitihada ambazo zimefanywa kuishauri Serikali kuhakikisha watoto wetu wanafundishwa maadili,” alisema Poleka.

Alisema, mbali na jitihada hizo, bado anaamini kuna haja ya kuendelea kutafuta njia nyingine ikiwemo kuanzisha program kwenye Vyuo Vikuu, na wamepata fursa ya kuvishauri vyuo vikuu mbalimbali kuona umuhimu wa suala hilo.

Alisema, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tayari wameanza kufundisha maadili na wamefanya mazungumzo na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) na Mzumbe ambao wanaangalia namna ya kulianzisha.

“Tunashukuru vyuo vingi vimeanza kuona umuhimu wa somo hilo, pia mbali na suala hilo, tunafanya tafiti ya vihatarishi vya uvunjaji wa maadili; tunaingia kwenye taasisi na tunaangalia vitu gani vinahatarisha uvunjifu wa maadili na kuwashauri namna ya kuzuia tatizo lisitokee,” alisema Pokela.

Aidha, alisema jitihada nyingine wanazozifanya ili kukuza maadili nchini, ni kusimamia uwekwaji saini viapo vya uadilifu na mwenendo na uadilifu wa viongozi na tayari Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wameandaa mwongozo kwa ajili ya kuangalia maisha ya viongozi.

“Tunaangalia mwenendo wao kuanzia nyumbani, mtaani na kwingineko ili tuweze kushauri Mamlaka kuhusu eneo hilo. Maadili ni jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi na jamii nzima, wanahabari mna jukumu kubwa kwenye jambo hilo,” alisisitiza Pokela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here