📌 Waipongeza REA utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umetoa wito kwa viongozi wa dini nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kulinda afya na kuokoa mazingira.
Rai hiyo imetolewa Agosti 13, 2025 katika Mji mdogo wa Majimoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kwa viongozi wa dini wapatao 240 na Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt.Joseph Sambali wakati wa semina iliyoandaliwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya kuwakumbusha nafasi zao katika jamii hususan kuhusu umuhimu wa kutunza amani, utulivu na maadili katika jamii.

“Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kutokana na nafasi yenu katika jamii; jambo hili mkilipa kipaumbele itasaidia kubadilisha fikra za jamii kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia,” alisisitiza Dkt. Sambali.
Alifafanua kuwa, REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ambao umeelekeza ifikapo mwaka 2034; 80% ya wananchi wawe wanatumia Nishati safi ya Kupikia.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaj Majid Mwanga ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema viongozi wa dini ni kiungo muhimu katika kutunza na kulinda amani, utulivu, maadili na uhifadhi wa mazingira kwa ustawi wa jamii nzima.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Shamim Mwariko alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya ununuzi wa majiko ya gesi (LPG) yanayosambazwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa ufadhili wa Serikali wilayani hapo.
“Viongozi wa dini tunahitaji ushiriki wenu katika Kampeni hii ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kulinda afya na kuokoa mazingira kwani kwa kufanya hivyo itachangia kuleta amani, utulivu na maadili katika jamii,” alisisitiza Mwariko.
Kwa nyakati tofauti, wakichangia katika semina hiyo, viongozi wa dini waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni kuunga mkono ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
“Ajenda hii ya Nishati Safi ya Kupikia imekuja kwa wakati mwafaka kutokana na kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa pia na ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa,” alisema Sheikh wa Wilaya ya Mlele, Awamu Muzamiru.
“Tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa dini, tumejadili mambo mengi na tunaahidi haya yote tuliyofahamishwa katika semina hii tutakuwa mabalozi wazuri kwa jamii,” alisema Mchungaji kutoka Kanisa la TAG Kijiji cha Kitupa, Paschal Katema.
Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia (2024-2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatumia njia mbalimbali katika kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika jamii.