Na Mwandishi Wetu – WMTH Bungeni, Dodoma
SERIKALI imejumuisha Vijiji vya Mnyamasi na Kasisi vilivyopo katika Kata ya Ugalla, Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, katika mradi mpya wa mawasiliano ya simu unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika Robo ya Nne ya mwaka wa fedha 2026/27.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Anna Richard Lupembe, aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga mnara wa mawasiliano katika Kijiji cha Mnyamasi.
Akifafanua hatua zilizochukuliwa, Dkt. Mkama amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ilikijumuisha Kijiji cha Mnyamasi katika Mradi wa Mawasiliano Vijijini Awamu ya Tatu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu maeneo ya vijijini.
Amesema kupitia mradi huo, kampuni ya mawasiliano ya Halotel ilijenga mnara katika Kijiji cha Katambike, ambao unahudumia vijiji vya Kasisi, Katambike na Mnyamasi.
Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na Serikali kupitia UCSAF ilibaini kuwa kuna umbali mkubwa kati ya mnara huo na Kijiji cha Mnyamasi, hali inayochangia changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu kwa wakazi wa eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imejumuisha Vijiji vya Mnyamasi na Kasisi katika mradi mpya wa mawasiliano unaotarajiwa kuanza kutekelezwa katika Robo ya Nne ya mwaka wa fedha 2026/27, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo husika.