Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba.
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba amesema Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NEST) umewezesha kutolewa kwa zabuni 403,643 zenye thamani ya Shilingi trilioni 42.6.
Simba alisema hayo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya PPRA na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), ambapo aliweka wazi kwamba, mfumo huo umeimarisha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma, ambapo kiwango cha uzingatiaji kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 79 mwaka 2025/26.
Alisema, NEST imepunguza gharama na muda wa kushiriki zabuni kwa kuwawezesha wazabuni kuwasilisha maombi kwa njia ya kielektroniki bila kulazimika kusafiri kwenda kwenye taasisi nunuzi.
“Mfumo wa NeST umeondoa ulazima wa wazabuni kusafiri kupeleka nyaraka za zabuni kwa Taasisi nunuzi. Hatua hii pia imepunguza gharama na muda wa kushiriki michakato ya ununuzi wa umma. Hivi sasa, mzabuni anaomba zabuni popote alipo,” alisema.
Simba aliongeza kuwa, matumizi ya Mfumo wa NeST yamewezesha kuwa na ushiriki mkubwa zaidi wa wazabuni, kwa kutoa zabuni kuanzia ngazi ya juu, ya kati hadi ngazi ya msingi (Serikali za Mitaa).
“Hivi sasa, kupitia Mfumo wa NeST, hata mafundi wa kawaida tu wanaweza kuomba na kupata kazi ya kushiriki ujenzi katika miradi ya Serikali. Pia, zabuni za hadi ngazi ya msingi, zinatolewa kwa haki na usawa kupitia Mfumo wa NeST. Hapa nazungumzia ununuzi katika ngazi za shule, vituo vya afya, ofisi za kata n.k,” alisema.
Aidha, alisema makundi maalumu yamepata zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 82.34, zikiwemo za vijana Shilingi bilioni 44.74, wanawake Shilingi bilioni 33.51, wazee Shilingi bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Shilingi milioni 680.
“Lengo la PPRA, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni kuwa na takribani makundi 300,000 yaliyo tayari kuomba zabuni. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kutoa ajira na kazi kwa Watanzania ambao hawana uwezo wa kuwa na kampuni, ambao wanaweza kujiunga kwenye vikundi na kutekeleza zabuni husika,” alisema Simba.
Alisema, kutokana na nia ya kuwainua Watanzania kiuchumi, Kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Shilingi Milioni 500, pia kutokana na umuhimu wa suala hili, Serikali iliweka sehemu ya ajenda muhimu kwenye Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu. Hatua iliyoongeza usajili wa vikundi, hamasa na utekelezaji wa utoaji wa zabuni.
“Nichukue fursa hii kuishukuru Ofisi ya Rais – Wizara ya Maendelea ya Vijana kwa kuridhia ombi letu la kushhirikiana nao kwenye jambo hili ambapo tulizunguka nao katika Halmashauri zote 184 nchini ambapo mwenge ulihitimishwa tarehe 14 Okitoba kule Mkoa wa Rukwa lakini sisi tunaendelea na uhamasishaji na Usajili wa Makundi hayo,” alisema.
Kupitia nafasi hiyo, Mkurugenzi huyo wa PPRA aliwasihi Watanzania kuendelea kujiunga kwenye vikundi vya watu watatu na kuendelea kuvisajili kwenye Halmashauri, na kisha wasajili kwenye Mfumo wa NeST ambao ndio wenye zabuni zote za umma.
“Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na uchumi jumuishi; kwamba kila Mtanzania ananufaika na anachangia pia kwenye ukuaji wa uchumi katika ngazi yoyote aliyopo,” alisema na kuongeza kuwa, hadi sasa makundi 33,659 yamesajiliwa katika mfumo huo, huku PPRA ikiendelea kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi na kujisajili ili kunufaika na fursa za ununuzi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato, alisema PPRA ina jukumu muhimu katika kusimamia ununuzi wa umma kwa kuzingatia uwazi, ushindani na uwajibikaji.
Alisema, ushirikiano kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari ni muhimu katika kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu fursa za kiuchumi, huku ununuzi wa umma ukiendelea kuwa nyenzo ya kukuza biashara za ndani, kuongeza ajira na kupanua ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya nchi.