‘Vijiji 80 vimeshapelekewa umeme vimebaki vijiji 4 tu’

0
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

?Naibu Waziri Kapinga aahidi kila Kitongoji kitafikiwa na umeme

Na Veronica Simba

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imefanikiwa kufikisha umeme katika Vijiji 80 kati ya Vijiji 84 katika Wilaya ya Singida ikiwa ni dhamira ya Serikali kuendelea kuwafikishia maendeleo wananchi wa vijijini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati wa ziara yake Juni 5 ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Mdilu na Mwasauya Kata ya Mwasauya wilayani Singida mkoani Singida na kuahidi kuwa vijiji vilivyobaki vitapata umeme kabla ya mwezi Juni kuisha.

“Ndugu zangu kazi nzuri hii mnayoiona ni matunda ya uchapakazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maono yake ndiyo yaliyopelekea vijiji vyote Tanzania hii kuweza kupelekewa umeme ikiwemo vijiji katika Jimbo la Singida Kaskazini.

Leo tulivyofika hapa, katika vijiji 84, vijiji 80 vimeshapelekewa umeme vimebaki vijiji 4 tu na katika vijiji hivyo 4 kazi inaendelea na muda siyo mrefu vitaunganishwa na umeme,” alisema Naibu Waziri Kapinga.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi na kusisitiza kuwa safari ya kupeleka umeme katika vitongoji imeanza na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na serikali yao pamoja na viongozi kwa kuwa maendeleo ni hatua.

“Serikali ya Awamu ya Sita tuliahidi na tunatenda. Nafahamu kuna vitongoji havina umeme. Lakini ndugu zangu maendeleo ni hatua. Ilikuwa ni lazima tufikishe miundombinu ya umeme kwenye vijiji ili sasa tuendelee na vitongoji.

Ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote na ndiyo maana kwenye mwaka wa fedha unaokuja, tumetenga fedha kupeleka umeme kwenye vitongoji 4,000. Niwahakikishie awamu kwa awamu, hatua kwa hatua vitongoji vyote vitapata umeme” alisisitiza Kapinga.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe alisema umeme umeleta maendeleo makubwa katika vijiji vilivyopo katika wilaya yake, ikiwamo kuwasaidia wanawake kutotumia muda mrefu kutafuta mashine za kusaga sababu ya uwekezaji wa mashine hizo katika vijiji vyao.

Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Miradi ambaye pia alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena alisema, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 80 kupeleka umeme katika vijiji Mkoani Singida huku akisema kuwa safari ya kupeleka umeme katika vitongoji katika mkoa huo imeshaanza.

“Wilaya hiyo ya Singida Vijijini ina jumla ya vitongoji 439, na katika vitongoji hivyo, 275 vimefikiwa na umeme,” alibainisha Mhandisi Lwena.

Naye Mbunge wa Singida Kaskazini, Abeid Ighondo kwa niaba ya wananchi amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoifikisha katika Jimbo hilo ikiwemo miradi ya umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here