KIJIJI cha Ruko, kilichopo katika Kata ya Kitwechenkura, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, mpakani mwa Tanzania na Rwanda, kimeanza kunufaika na huduma za mawasiliano baada ya kuunganishwa na mtandao wa simu kufuatia ujenzi wa minara 758 nchini.
Ruko ni kijiji kinachotegemea zaidi kilimo cha ndizi, mazao mengine ya biashara pamoja na shughuli za uvuvi.
Hata hivyo, kwa miaka kadhaa iliyopita, wakazi wake walikumbwa na changamoto ya kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika, hali iliyodhoofisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kupitia mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano, kijiji hicho sasa kimefikiwa na huduma za mtandao na kampuni ya simu ya Yas Tanzania, kwa ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia UCSAF.
Aidha, huduma za kifedha kwa njia ya simu zimeimarika, kurahisisha kutuma na kupokea fedha bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki.
Kwa ujumla, ujio wa mawasiliano ya uhakika umeonekana kuwa chachu ya maendeleo katika kijiji cha Ruko.